Wanajeshi wa Ufaransa kutimuliwa pia nchini Senegal
Ufaransa na Senegal zimeeleza kuwa zimeamua kuunda tume ikiwa ni katika fremu ya maandalizi ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Imeelezwa kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wanapaswa kuondoka nchini Senegal ifikapo mwisho mwa mwaka huu.
Taarifa ya pamoja ya nchi hizo imeeleza kuwa, Senegal na Ufaransa zimeazimia kufanya kazi kuelekea kuwa na ubia katika ulinzi na usalama unaozingatia vipaumbele vya kimkakati vya pande zote.
Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal mwaka jana (2024) alitangaza kuwa, Ufaransa ina inapaswa kufunga kambi zake zote za kijeshi katika nchi hiyo na kuondoa wanajeshi wake nchini humo. "Karibuni hivi wanajeshi wa Ufaransa hawatakuwepo Senegal," Faye aliliambia gazeti la Le Monde mwezi Novemba mwaka jana ambapo alitilia mkazo umuhimu wa mamlaka ya kitaifa nay a kujitawala nchi hiyo.
Matamshi hayo ya Rais Faye wa Senegal yalikuwa ya kwanza kuwahi kutolewa na serikali ya nchi hiyo kuhusu suala la kuondoka nchini humo wanajeshi wa Ufaransa.
Wanajeshi wa Ufaransa wameendelea kuwepo nchini Senegal tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1960, hususan katika uga wa mafunzo na kile kinachoelezwa kama operesheni za usalama za kikanda.
Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko mwezi Mei mwaka jana (2024) alikosoa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo na akasisitiza ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Uamuzi huo unaifanya Senegal kuwa nchi ya tano barani Afrika kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa na kufunga kambi zake za kijeshi. Hapo awali, nchi za Mali, Niger na Burkina Faso zilivifukuza vikosi vya Ufaransa na kufunga vituo vyao vya kijeshi. Hii ni katika hali ambayo, Ufaransa inatarajiwa kuondoa vikosi vyake vya kijeshi kutoka Ivory Coast huko Afrika Magharibi mnamo Februari 20 ikiwa ni muendelezo wa kupata pigo Ufaransa katika makoloni yake ya zamani.
Kwa kufukuzwa vikosi vya jeshi la Ufaransa kutoka nchi za Kiafrika, inaweza kusemwa kwamba, kipindi cha ukoloni mamboleo, ambacho kiliwekwa na nchi za kikoloni baada ya uhuru wa nchi za Kiafrika, kinaelekea ukingoni, na serikali za Kiafrika zinajaribu kuanzisha kipindi kipya cha utawala wa kisiasa kwa msingi wa uhuru kamili na mamlaka ya kujitawala.
Kuongezeka mwamko wa watu wa Afrika, haswa kizazi cha vijana waliosoma, pamoja na utekelezaji wa wazo la uhuru wa kisiasa na kiuchumi na kuhisi udhalili kutokana na uwepo wa majeshi ya kikoloni, kumesababisha nchi za Kiafrika kuchukua hatua ya kuyafukuza majeshi ya Ufaransa.
Ukweli ni kwamba kati ya nchi makoloni ya zamani zikiwemo Uingereza, Ureno na Italia, dola la Ufaransa lilifanya unyama na ukatili mkubwa zaidi katika nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wake. Kiasi kwamba, nchi hizo hazijaruhusiwa kupata ustawi na maendeleo hata kidogo. Kwa muktadha huo, nchi zilizokoloniwa na Ufaransa zinahesabiwa kuwa zilizobakia nyuma sana kimaendeleo.
Mauaji na vitendo vya jinai vya Ufaransa katika nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wake vimekuwa vikitokea kila mara ili kunyamazisha sauti yoyote ya upinzani dhidi ya uwepo wa jeshi la Ufaransa. Mintarafu hiyo ukoloni wa Ufaransa katika nchi za Kiafrika umesababisha uharibifu mkubwa usioweza kufidika wa kimwili, kiakili, kihisia na kimaada, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa kiuchumi, uzalishaji bidhaa na sekta ya viwanda.
Ni kwa kuzingati ukweli huo ndio maana, nchi za Kiafrika zina matumaini kwamba, kwa kutimuliwa wavamizi katika nchi zao zifungue ukurasa mpya wa maendeleo na ustawi kwa kutegemnea wazawa na vigezo vya kikanda na kieneo. Kile ambacho ni muhimu katika kuendelea na mchakato huu ni kwamba, nchi za Kiafrika zinapaswa kuwa macho na makini zisije zikatumbukia katika hila na mitego ya mikataba na hati mpya za makubaliano ya kiusalama na nchi za Magharibi, ikiwemo Ufaransa, kwa sababu hilo litapelekea kuendelea ukoloni kwa mtindo mpya.