Kumalizika mkutano wa 38 wa wakuu Umoja wa Afrika Addis Ababa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122824-kumalizika_mkutano_wa_38_wa_wakuu_umoja_wa_afrika_addis_ababa
Mkutano wa 38 wakuu wa Umoja wa Afrika ulimalizika jana katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia.
(last modified 2025-02-16T23:04:02+00:00 )
Feb 16, 2025 23:04 UTC
  • Kumalizika mkutano wa 38 wa wakuu Umoja wa Afrika Addis Ababa

Mkutano wa 38 wakuu wa Umoja wa Afrika ulimalizika jana katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia.

Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali muhimu ya kikanda na bara, ikiwemo amani na usalama, uchumi, na mageuzi ya kitaasisi.

Kadhalika viongozi wa Afrika wamejadili hali ya amani na usalama, Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, mageuzi ya kitaasisi katika jumuiya hiyo na masuala mengine ya kimkakati.

Katika mkutano wao huo, viongozi wa Afrika pia wamezindua juhudi mpya za fidia zinazohusiana na utumwa na ukoloni, na kaulimbiu ya mwaka huu, "Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia," ikilenga kushughulikia dhuluma za kihistoria na athari zake za kudumu barani Afrika.

Mpango huu unalenga kupata fidia za kifedha, kukiri rasmi makosa ya zamani, na mageuzi ya sera kutoka kwa mataifa ya kikoloni

Viongozi wa mataifa ya Afrika walikutana katika mkutano wa kilele wa siku mbili wa Umoja wa uliofanyika chini ya wingu zito la mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na vita nchini Sudan.

Baadhi ya wakuu wa Umoja wa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja

 

Mkutano huo ulifunguliwa siku ya Jumamosi huku juhudi za kidiplomasia kuutatua mzozo wa mashariki mwa DRC zikigonga ukuta ambapo waasi wa M23 waliendelea kusonga mbele baada ya kuudhibiti mji mwingine mkubwa wa  Bukavu  mashariki mwa nchi hiyo.

Rais wa Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hakushiriki mkutano huo lakini amewakilishwa na Waziri Mkuu, Judith Suminwa Tuluka.

Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, amechukua uenyekiti wa kupokezana wa Umoja wa Afrika (AU) na kuahidi kuzishughulikia changamoto za kiusalama barani humo.

Moja ya zilizokuwa ajenda kuu za mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika ilikuwa ni kumchagua Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika atakayerithi mikoba ya Moussa Faki Mahamat anayemaliza muda wake. Wagombea watatu akiwemo mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga walijitokeza kuwania nafasi hiyo muhimu katika Umoja wa Afrika.

Mahamoud Ali Youssouf Ali Youssouf, Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti ameibuka mshindi baada ya kuwapiku washindani wake.

Youssouf alishinda kwa kupata kura 33 katika raundi ya 7, ambayo alisalia kama mgombea pekee baada ya Raila kujiondoa katika raundi ya sita kufuatia kupitwa kura na Youssof katika raundi ya tatu, nne, tano na raundi hiyo ya sita.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anakabiliwa kibarua kigumu ambapo mbele yake kwa sasa kuna changamoto kubwa kama vita vya Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tawala za kijeshi katika eneo la Afrika Magharibi, mdororo wa uchumi, na mabadiliko ya tabianchi.

Hasa kwa kutilia maanani kwamba, baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema, mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, unaweza kusababisha vita vya kikanda.

Mahamoud Ali Youssouf Ali Youssouf, Mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika

 

Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye nchi yake inanyooshewa kidole cha lawama cha kuwaunga mkono waasi wa M23 alihudhuria mkutano huo mjini Addis Ababa.

Licha ya kuwa nchi yake inakana kuwaunga mkono waasi hao, lakini duru mbalimbali za kieneo na kimataifa zikiwemo ripoti za Umoja wa Mataifa zinasisitiza juu ya kupata himaya waasi hao kutoka Rwanda.

Mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika umemalizika na kutolewa maazimio kadhaa kuhusiana na masuala mbalimbali yanayoligubika bara la Afrika hivi sasa katika hali ambayo, asasi hiyo imekuwa ikiandamwa na ukosoaji kutokana na kutokuwa na misimamo thabiti katika kushughulikia migogoro ya bara hilo.

Wachambuzi wa mambo wanasema, taasisi hiyo kubwa zaidi barani Afrika inapaswa kuwa na misimamo imara na kushughulikia kwa haraka na bila kusuasua changamoto zinazolikabili bara hilo hasa vita na machafuko.

Filihali ni kusubiri na kuona ni kwa namna gani maazimio na maamuzi ya mara hii yaliyopasishwa katika mkutano wa 38 wa wakuu wa Umoja wa Afrika yatafanyiwa kazi na hivyo kumaliza au kwa akali kupunguza changamoto na matatizo yanayolikabili bara la Afrika.