Uganda yatuma vikosi zaidi nchini DRC, yathibitisha kuwa wanajeshi wake wameingia Bunia
Msemaji wa Jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulayigye amethibitisha kuwa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (UPDF) limeingia kwenye eneo la Bunia, ambalo ni makao makuu ya jimbo la Ituri, sehemu muhimu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
Jenerali Kulayigye amevieleza vyombo vya habari kuwa UPDF inalenga kuwadhibiti wanamgambo wa ADF ambao wana uhusiano na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) na ambao wanaendeleza mauaji ya watu katika kanda hiyo.
Jeshi la Uganda, kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC), limeendelea kukisaka kikundi cha waasi hao ambao wametokea Uganda na kupiga kambi katika misitu ya Kongo DR.
Itakumbukwa kuwa, Mkuu wa Majeshi ya Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni, alitoa onyo mwishoni mwa juma kuwa jeshi hilo lingeshambulia eneo la Bunia, iwapo vikosi vya wapiganaji wa ADF vitakaidi kujisalimisha ndani ya saa 24.
Hayo yanajiri wakati Uganda inaandamwa na lawama za kuhusika na mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Licha ya kuwepo vikosi vya UPDF mashariki mwa DRC kusaidia majeshi ya serikali dhidi ya ADF, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Uganda imehusika na utoaji mafunzo kwa wapiganaji wa kundi la waasi la M23.
Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na serikali ya Kampala.../