M23 yatishia kulipiza kisasi dhidi ya jeshi la serikali ya DRC, yadai linashambulia raia Walikale
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124766-m23_yatishia_kulipiza_kisasi_dhidi_ya_jeshi_la_serikali_ya_drc_yadai_linashambulia_raia_walikale
Kundi la waasi la M23 limetishia kulipiza kisasi iwapo majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yataendelea kushambulia raia katika eneo la Walikale.
(last modified 2025-04-05T02:36:26+00:00 )
Apr 05, 2025 02:36 UTC
  • M23 yatishia kulipiza kisasi dhidi ya jeshi la serikali ya DRC, yadai linashambulia raia Walikale

Kundi la waasi la M23 limetishia kulipiza kisasi iwapo majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yataendelea kushambulia raia katika eneo la Walikale.

Msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka ameeleza katika andiko aliloweka kwenye ukurasa wa X kuwa wapo tayari kujibu mashambulizi iwapo majeshi ya serikali yataendelea kushambulia raia.

“Ikiwa majeshi ya Kinshasa yataendelea na uchokozi wao dhidi ya raia, nasi tuko tayari kukabiliana na vitisho hivyo,” amesisitiza Kanyuka.

Mnamo Machi 19, waasi wa M23 hao waliudhibiti mji wa Walikale ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu, lakini wakajiondoa ili kutii agizo la kusitisha mapigano lililotolewa Februari 22.

Uamuzi wa kuweka silaha chini, kulingana na waasi hao, ulilenga kuunga mkono jitihada za amani, katika eneo la mashariki mwa DRC.

Katika taarifa yake ya Machi 24, Kanyuka alisisitiza kuwa uwepo wa majeshi ya DRC, unatatiza jitihada za kumaliza mapigano katika eneo hilo.

Siku ya Alkhamisi, gavana wa zamani wa jimbo la Sankuru, Joseph Stephane Mukumadi alijiunga na waasi hao, huku akitoa wito kwa Wakongomani kuungana na kuundoa aliouita utawala wa kidikteta nchini humo.../