Machar apokonywa uongozi wa upinzani Sudan Kusini akiwa kizuizini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124980-machar_apokonywa_uongozi_wa_upinzani_sudan_kusini_akiwa_kizuizini
Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini, Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition (SPLM-IO), siku ya Jumatano kilimteua mwenyekiti wa mpito huku Makamu wa Kwanza wa Rais wa chama hicho, Riek Machar, akiendelea kuzuiliwa nyumbani.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 10, 2025 04:14 UTC
  • Machar apokonywa uongozi wa upinzani Sudan Kusini akiwa kizuizini

Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini, Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition (SPLM-IO), siku ya Jumatano kilimteua mwenyekiti wa mpito huku Makamu wa Kwanza wa Rais wa chama hicho, Riek Machar, akiendelea kuzuiliwa nyumbani.

Machar alizuiliwa nyumbani na Rais Salva Kiir Mayardit mwezi uliopita.

Baraza la Ukombozi wa Kitaifa  katika  chama hicho lilimpendekeza na kumuidhinisha Stephen Par Kuol, waziri wa ujenzi wa amani katika serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa, kuwa mwenyekiti wa muda hadi Machar atakapoachiliwa.

Akizungumza katika mkutano wa mashauriano uliofanyika katika mji mkuu, Jubam Kuol amesema:"Tukiendelea mbele, SPLM-IO inasalia thabiti katika dhamira yetu ya kutetea haki na heshima ya wananchi wote wa Sudan Kusini, na kujenga mustakabali wa amani, umoja na maridhiano."

Alieleza kuwa chama hicho kimejitenga rasmi na Nathaniel Oyet Pierino, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama hicho ambaye kwa sasa yuko uhamishoni.

Wakati huohuo, Losuba Ludoru Wongo ameteuliwa kuwa naibu mwenyekiti huku Agok Makur Kur akichukua nafasi ya Katibu Mkuu wa chama.

Kuol amebaini kuwa: “Chama ambacho ni sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa hakiwezi kuongozwa au kupokea maagizo kutoka kwa viongozi walio uhamishoni. Maamuzi ya chama na serikali hufanyika katika makao rasmi ya taasisi hizo, si kwa njia ya mbali."

Amesisitiza tena dhamira yao ya kutekeleza kwa dhati na kwa ukamilifu makubaliano ya amani ya mwaka 2018. Aidha amesema: “Tunaamini kwamba makubaliano haya ndiyo njia pekee ya kufanikisha amani ya kudumu na maridhiano miongoni mwa jamii mbalimbali za Sudan Kusini."

Sudan Kusini, taifa tajiri kwa mafuta, lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru mwaka 2011, lakini likajikuta kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili baadaye.

Utekelezaji wa makubaliano ya amani ya 2018 umekuwa wa polepole, huku hali ya taharuki ikiongezeka kufuatia mapigano ya hivi karibuni kati ya kikundi cha waasi kinachojiita White Army, kinachoaminika kuwa na uhusiano na Machar. Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kwamba Naibu Rais wa Kwanza, Riek Machar, amekamatwa na atachunguzwa kwa tuhuma za kujaribu kuchochea uasi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema anasikitishwa sana na kuendelea kushtadi taharuki na hali ya mambo nchini Sudan Kusini.

Kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba, nchi hiyo ya Kiafrika ipo katika ncha ya kutumbukia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.