Pande hasimu Sudan zatakiwa kulinda usalama wa raia
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imezitaka pande hasimu nchini Sudan kulinda usalama wa raia na kurahisisha kufikiwa na misaada ya kibinadamu maeneo ya mapigano ili kuepusha majanga zaidi ya kibinadamu nchini humo.
Katika ripoti iliyotolewa Alkhamisi, ICRC imesema kuwa usalama wa raia na kutokwamishwa misaada kuwafikia wahanga wa vita ni wajibu wa kisheria na ndiyo njia pekee ya kuepusha kuzorota zaidi hali ya kibinadamu nchini Sudan.
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu aidha limezikumbusha pande hasimu nchii Sudan ahadi zao ndani ya Azimio la Jeddah la mwaka 2023 ambapo pande zote zilitia saini makubaliano ya kuheshimu sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu.
ICRC imeoonya kwamba kutoheshimiwa sheria za kimataifa za kibinadamu umechangia katika mgogoro huo na kupungua kwa kiasi kikubwa ufadhili wa kimataifa kunahatarisha zaidi maisha ya wahanga wa vita nchini Sudan.
Imeongeza kuwa, wastani wa asilimia 70 hadi 80 ya vituo vya afya katika maeneo yaliyoathiriwa na vita nchini Sudan havifanyi kazi tena na hivi sasa wastani wa kila raia wawili kati ya watatu hawapati huduma za matibabu kwenye maeneo hayo.
Sudan imekuwa katika mzozo mbaya vita unaotokana na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Hadi hivi sasa watu 29,683 wameripotiwa kupoteza maisha kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Nalo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema kuwa, vita vya Sudan vimewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 15, ndani na nje ya nchi hiyo.