Mamilioni wanatarajiwa shughuli ya kumuaga Kiongozi Shahidi nchini Iraq
-
Saad Maan msemaji wa kamati ya vyombo vya habari inayoratibu hafla ya shughuli ya mazishi ya Kiongozi Shahidi Iraq
Mamilioni ya waumini wanatarajiwa kufurika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala nchini Iraq kushiriki katika shughuli za mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa kamati ya vyombo vya habari inayoratibu hafla hiyo nchini Iraq.
Luteni Jenerali Saad Maan, msemaji wa kamati hiyo, amesema msafara wa mazishi utafika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala, huku kukiwa hakuna shughuli zilizopangwa Baghdad kutokana na ufinyu wa muda.
Maan aliambia mkutano na waandishi wa habari kuwa, makadirio ya awali yanaashiria kuwa mamilioni ya watu watashiriki katika msafara wa mazishi ya Shahid Ayatullah Khamenei nchini Iraq.
Amesisitiza kuwa miundombinu na rasilimali zote muhimu zimeandaliwa ili kuhakikisha utulivu na usalama, akitoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzi.
Maan ameongeza kuwa vikao vya maandalizi vinaendelea na mamlaka husika ziko katika utayari wa hali ya juu. “Tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha mpango madhubuti wa kuratibu shughuli hizi za mazishi,” alisema, akiahidi kutoa maelezo zaidi ya kina katika mkutano utakaofanyika Jumapili au Jumatatu.
Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran pia imetangaza utayari wake kutoa huduma za dharura na afya wakati wote wa shguhuli za mazishi nchini Iran na Iraq.
Mapema Alhamisi, msemaji wa wakuu wa majeshi ya Iraq alisema kuwa “mwili mtukufu” wa Kiongozi Shahidi utasindikizwa kutoka Kufa kuelekea Najaf saa 12:00 asubuhi, Julai 8, “kwa kushirikisha mamilioni ya Wairaqi.”
“Saa 10:00 jioni, mwili utapita katika sehemu za mji mtakatifu wa Karbala kabla ya ibada za mwisho kufanyika katika Haram za Imam Hussein (AS) na ndugu yake Abu al-Fadl al-Abbas (AS),” Jenerali Maan alibainisha.
Aidha, amegusia kuwa jumbe za kigeni zitakuwepo katika msafara huo. Siku ya Jumanne, kituo cha televisheni cha Alhurra kiliripoti kuwa Kamati ya Arbaeen ya Iraq imepewa dhamana ya kusimamia shughuli hizi za kihistoria.