Mkuu wa Kamisheni ya AU atoa mwito wa kukomeshwa mapigano nchini Sudan
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka ghasia nchini Sudan, hasa katika eneo la Darfur Kaskazini.
Youssouf ameelezea kusikitishwa na hali ilivyo hivi sasa wakati alipokuwa anatoa ripoti za mashambulizi makali karibu na El Fasher ikiwa ni pamoja na mashambulizi mabaya katika kambi za wakimbizi za Zamzam na Abu Shouk.
"Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya raia, ikiwa ni pamoja na watoto wadogo na wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu," amesema Youssouf na kuzitaja ghasia hizo kuwa ni ukiukaji usiokubalika na mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
Mkuu huyo wa AUC pia alitoa rambirambi kwa familia za wahanga na watu wa Sudan, akitoa mwito wa kukomeshwa mara moja vita hivyo vya kiuadui bila ya masharti yoyote. Amewataka wale waliouzingira mji wa El Fasher kuondoa kizuizi na kuruhusu kufikishwa vizuri misaada ya kibinadamu kwa wahanga wote.
Umoja wa Afrika umegusia pia taarifa za huko nyuma za Baraza la Amani na Usalama la umoja huo na kusisitizia haja ya dharura ya kupunguza mzozo ili kulinda raia na kurejesha amani na kuzitaka pande zote kujizuia na kuepuka vitendo vinavyoweza kuzidisha hali ya wasiwasi kwenye eneo hilo.
Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi la Sudan kwa ajili ya kudhibiti nchi. Vita hivyo vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi yameshasababisha maelfu ya vifo na kuufanya mgogoro huo kuwa miongoni mwa migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Zaidi ya watu 20,000 wameshauawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na serikali za mitaa.