Kenya yatupilia mbali madai ya Sudan kwamba inaunga mkono RSF
Serikali ya Kenya imekanusha madai yaliyotolewa na uongozi wa kijeshi nchini Sudan unaoilaumu Nairobi kwa mzozo unaoendelea nchini Sudan na kuwa nchi hiyo inaunga mkono kundi la RSF.
Wizara ya Mambo ya nje ya Kenya imeyataja madai hayo yanayosambazwa na uongozi huo wa kijeshi kuwa hayana msingi na ikasisitiza kwamba, lengo la Kenya ni kuona amani imepatikana nchini Sudan.
Kadhalika taarifa hiyo imesema kuwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, wakati huu mamilioni ya raia wakiyahama makazi yao huku misaada ikiwa inayotolewa ikiwa haikidhi mahitaji.
Kenya inasema imefanya juhudi za amani za kikanda na imefanya mikutano na makundi hasimu ya Sudan mjini Nairobi na katika maeneo mengine bila kuegemea upande wowote.
Huko nyuma Kenya imewahi kukosolewa na kulauumiwa na Sudan pamoja na wakosoaji nchini humo kwa kutowajibika kutokana na hatua ya kuwakaribisha waasi wa kijeshi wa Sudan ambao walipanga kutangaza serikali nchini mwao.

Kiongozi wa Sudan Abdul-Fattah al-Burhan alielezwa kushangazwa na hatua hiyo ya Kenya.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan ilikosoa serikali ya Rais William Ruto kwa kuruhusu tukio hilo.
Katika taarifa yake wizara hiyo imesema hatua hiyo inakuza mpasuko wa mataifa ya Kiafrika, inakiuka uhuru wao, na kuingilia mambo yao ya ndani.
Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) zimekuwa zikipigana vita tangu katikati ya Aprili 2023 ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na wengine milioni 14 kulazimika kuyahama makazi yao.