Wanajeshi wa Israel hawataki vita dhidi ya Gaza
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendelea kupinga vita dhidi ya Gaza.
Serikali ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu, imeendelea kukabiliwa na upinzani ndani ya jeshi kutokana na kuendelea kuweko upinzani wa kupinga vita dhidi ya Gaza.
Katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya askari wa akiba wa Israel - kutoka matawi yote ya jeshi - wametia saini barua wakiitaka serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusitisha mapigano na kujikita zaidi katika kufikia makubaliano ya kuwarudisha mateka waliosalia wanaoshikiliwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Miezi kumi na minane iliyopita, Waisrael wachache walitilia shaka mantiki ya vita: kuwashinda Hamas na kuwarudisha mateka.
Kwa wengi, usitishaji vita wa Januari na kurudi kwa mateka zaidi ya 30 kuliweka matumaini kwamba vita vinaweza kuisha hivi karibuni.
Lakini baada ya Israel kurejea vitani katikati ya mwezi Machi, matumaini hayo yalikatizwa.
"Tulifikia hitimisho kwamba Israel inaenda mahali pabaya sana," Danny Yatom, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Mossad alisema.
"Tunaelewa kwamba kinachomsumbua zaidi Netanyahu ni maslahi yake mwenyewe. Na katika orodha ya vipaumbele, maslahi yake na maslahi ya kuwa na serikali imara ndiyo ya kwanza, na sio mateka."
Wengi wa wale wanaotia saini barua za hivi majuzi ni, kama Yatom, wakosoaji wa muda mrefu wa waziri mkuu. Baadhi walihusika katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyotangulia kuzuka kwa vita tarehe 7 Oktoba 2023 kufuatia mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel.