UAE yaituhumu Sudan kusafirisha silaha kupitia nchi hiyo, Khartoum yakadhibisha madai hayo
(last modified Thu, 01 May 2025 05:55:43 GMT )
May 01, 2025 05:55 UTC
  • UAE yaituhumu Sudan kusafirisha silaha kupitia nchi hiyo, Khartoum yakadhibisha madai hayo

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetangaza kwamba umezuia jaribio haramu la kusafirisha mamilioni ya vifaa vya kijeshi na risasi kwa jeshi la Sudan katika moja ya viwanja vya ndege vya nchi hiyo.

Hata hivyo, jeshi la Sudan limeeleza kuwa ripoti hiyo ni ya uzushi inayolenga kuficha shutuma dhidi ya Abu Dhabi kwamba inunga mkono na kuwasaidia waasi wa Rapid Support Forces (RSF) katika vita vya umwagaji damu ambavyo vinaendelea nchini Sudan kwa takriban miaka miwili.

Mwanasheria Mkuu wa UAE ametangaza kuwa nchi hiyo imezuia jaribio la kusafirisha zana za kijeshi kwa ajili ya jeshi la Sudan na kukamatwa kile alichokitaja kuwa "kikundi kinachohusika na udalali na biashara haramu ya zana za kijeshi."

Al Shamsi amedai kuwa upande wa Mashtaka unaendelea kukamilisha upelelezi kwa ajili ya kesi hiyo na kwamba matokeo ya mwisho yatatangazwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Kwa upande wake, serikali ya Sudan imekanusha shutuma hizo za Imarati, ikisema "haizingatii madai hayo ya uzushi."

Khaled Al-Aiser, Waziri wa Utamaduni na Habari wa Sudan ambaye pia na msemaji rasmi wa serikali amesema: Serikali ya Sudan ina "uhakika kwamba Abu Dhabi inatumia vyombo vyake rasmi na vya kibinafsi kuzuia malalamiko yaliyowasilishwa na Khartoum katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikijua kwamba malalamiko haya yanatokana na ushahidi wa kutosha, ikiwa ni pamoja na harakati za ndege inayomilikiwa na Abu Dhabi, ambayo husafirisha silaha, vifaa na ndege zisizo na rubani kwa waasi wa RSF."

Kabla ya hapo Sudan ilikuwa imewasilisha kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikiishutumu UAE kuwapa silaha waasi wa RSF, madai ambayo yanaungwa mkono na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.