Jasusi wa MOSSAD nchini Iran anyongwa, mtandao wake wasambaratishwa
-
Mohsen Langarneshin
Katika pigo kubwa la kiusalama kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wake, Mahakama ya Iran imetangaza mapema leo Jumatano kwamba imetekeleza hukumu ya kunyongwa mmoja wa majasusi wakubwa wa shirika la ujasusi la Israel, MOSSAD.
Mhalifu huyo alipatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwa kuwa na nafasi muhimu katika operesheni kadhaa za kigaidi, hasa mauaji ya shahidi Kanali Hassan Sayyad Khodaei katikati mwa mji mkuu, Tehran.
Kituo cha Vyombo vya Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran kimeeleza kuwa jasusi aliyenyongwa, Mohsen Langarneshin, alikuwa chombo kichafu kilichokuwa mikononi mwa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni na alikuwa akishughulikia masuala ya kilojestiki na kiufundi kwa ajili ya utekelezaji wa operesheni za kigaidi ndani ya Iran, zikilenga vinara wa Muqawama na ulinzi wa nchi. Alikamatwa baada ya vyombo vya usalama kupenya kwenye usalama na kugundua uhusiano wake wa karibu na Mossad. Alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya uhaini (muharib) na kueneza ufisadi duniani, na hukumu ya kunyongwa kwake imetekelezwa alfajiri ya leo.

Taarifa ya Idara ya Mahakama ya Iran imesema, jasusi huyo aliajiriwa Oktoba 2020, na alipata mafunzo ya kina ya ujasusi na hujuma, na kuanza kazi yake ya kwanza Januari 2021 ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa Wazayuni wa kushambulia miundombinu ya ulinzi na usalama ya Iran.
Katika miaka miwili ya shughuli zake ovu ndani ya nchi, aliratibu na maafisa wakuu wa MOSSAD na kushiriki katika kupanga na kutekeleza hujuma za kigaidi, ikiwa ni pamoja na shambulio dhidi ya kituo cha viwanda cha Wizara ya Ulinzi huko Esfahan na mauaji ya Sayyad Khodaei.
Majukumu yake yalijumuisha kununua vifaa vya mawasiliano vilivyosimbwa, kutafuta nyumba salama katika mikoa kadhaa, kuhamisha fedha kutoka kwa viongozi wa MOSSAD hadi kwa maajenti wa shirika hilo, na kutoa magari na vifaa vya uchunguzi kwa timu za utekelezaji. Pia alifanya mikutano ya moja kwa moja na maafisa wa MOSSAD huko Georgia na Nepal, akipokea maagizo kutoka kwao ya jinsi ya kutekeleza jinai za mauaji na ujasusi.
Licha ya kupewa mafunzo ya hali ya juu na ujuzi wa masuala ya ujasusi, ajenti huyo wa MOSSAD aliangukia mikononi mwa maafisa wa kupambana na ujasusi, ambao walizima mipango yake na kusambaratisha mtandao wake wote. Baada ya kesi ya haki na ya uwazi, hukumu ya Mungu imetekelezwa asubuhi ya leo, na mhalifu huyo amekutana na hatima ya giza aliyostahili.