Tshisekedi atetea mkataba wa amani kati ya DRC na Rwanda
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ametetea mkataba uliotiwa saina baina ya nchi yake na Rwanda kwamba ni mwanzo mzuri wa kuleta amani mashariki mwa nchi yake.
Rais Felix Tshisekedi amesema hayo katika mkutano na waandishi habari mjini Kinshasa na kuongeza kuwa, ndoto yake ni kuona amani ya kudumu imerejea kwenye majimbo ya Kivu na Ituri.
'Ni kweli ni tangazo la nia njema, lakini ni hatua muhimu katika njia nzuri. Njia ambayo kila siku nimeitarajia kwa ajili ya amani ndani ya nchi yangu. Nitarudisha amani, lakini amani ya kweli na ya kudumu. Kutokana na kile mnachokiona, hakutakuwa na ukosefu wa utulivu tena katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo", alisema Tshisekedi.
Huku hayo yakijiri, Kamati ya kimataifa la Msalaba Mwekundu imetangaza kuanza zoezi la kuwasafirisha hadi mjini Kinshasa, mamia ya wanajeshi na maafisa wa polisi ya Kongo waliokwama mjini Goma, toka kutekwa kwa mji huo na waasi wa M23 miezi mitatu iliopita.
Wanajeshi hao walipewa hifadhi kwenye kambi ya Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, Monusco. Zoezi hilo ambalo litachukuwa sikuu kadhaa, limekuja baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Kongo na waasi M23. Kulingana na vyanzo vya Umoja wa Mataifa ni kwamba takriban wanajeshi 1,500 wa Kongo walipewa hifadhi kwenye kambi za Monusco, huko mjini Goma.