MSF: Vita nchini Sudan vimeharibu sekta ya afya
(last modified Sat, 10 May 2025 12:18:07 GMT )
May 10, 2025 12:18 UTC
  • MSF: Vita nchini Sudan vimeharibu sekta ya afya

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeonya kwamba hali ya afya katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, inazidi kuwa mbaya kutokana na vita, na kukosekana huduma za afya za kimsingi na za kuokoa maisha ya watu.

Katika taarifa yake iliyotolewa baada ya timu za shirika hilo kukutana na wafanyakazi wa Wizara ya Afya katika Hospitali ya Kufundishia ya Bashayer kusini mwa Khartoum, Suleiman Ammar, mratibu wa masuala ya matibabu wa MSF amesema kuwa vita vimekuwa na "athari mbaya kwa uwezo wa watu kupata huduma za afya huko Khartoum."

Ammar amesema kuwa wakazi wengi wa maeneo ndani ya mji mkuu, ikiwa ni pamoja na Khartoum Kusini, hawana huduma ya afya ya msingi ya kuokoa maisha.

"Timu yetu inafanya kazi katika Hospitali ya Kufundisha ya Bashayer ili kuhakikisha kitengo cha matibabu ya kipindupindu kiko tayari kupokea wagonjwa,"amesema afisa huyo na kuongeza, "Zaidi ya wafanyikazi 60 wa hospitali wamepatiwa mafunzo, vifaa vya matibabu maalumu vya kipindupindu vimefika, na tumeandaa vitanda 20."

Kwa upande wake, Claire San Filippo, mratibu wa dharura wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), ameeleza kuwa mahitaji ya huduma za afya huko Khartoum bado ni makubwa. Ametaja mlipuko wa sasa wa kipindupindu kuwa ni "moja ya changamoto zinazowakabili wakazi ambao bado wanaishi Khartoum au wanaorejea kutoka sehemu nyingine za nchi."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 20,000 wameuawa na milioni 15 wamepoteza makazi kutokana na vita vya ndani nchini Sudan. Hata hivyo, utafiti wa wataalamu unaeleza kuwa idadi ya vifo huenda imefikia takriban 130,000.