Charles Hillary, aliyewahi kuwa mtangazaji mahiri afariki dunia
(last modified Sun, 11 May 2025 04:33:37 GMT )
May 11, 2025 04:33 UTC
  • Charles Hillary, aliyewahi kuwa mtangazaji mahiri afariki dunia

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hilary, amefariki dunia alfajiri ya leo Mei 11, 2025.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu, Hilary amefariki baada ya kuugua ghafla na mauti yamemkuta akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila.

Marehemu Charles Hilary alizaliwa Zanzibar miaka 66 iliyopita eneo la Jang’ombe. Mwaka 1968 alihamia jijini Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Msingi ya Ilala Mchikichini.

Alijiunga na Redio Tanzania mwaka 1981 na kuitumikia hadi mwaka 1994 alipojiunga na kituo binafsi cha Radio One Stereo kinachomilikiwa na IPP.

Mwaka 2003 aliondoka nchini na kujiunga na Radio Deusch Welle (DW) nchini Ujerumani, na miaka mitatu baadaye alijiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa Idhaa ya Kiswahili.

Mwaka 2015 aliamua kurejea nchini na kujiunga Azam Media ambako alifanya kazi hadi mwaka 2023. Alihitimisha muda wake akiwa Mkuu wa Idara ya redio ya UFM, baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.