Watu 33 wauawa katika mashambulizi yanayoshukiwa kuwa ya RSF nchini Sudan
Takriban watu 33 wameuawa nchini Sudan katika mashambulio yanayoshukiwa kufanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huku vita vya kikatili vya miaka miwili vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vikiendelea kuchukuka roho za watu na kuinakamisha Sudan.
Taarifa zinasema kukwa shambulio la RSF kwenye gereza la el-Obeid la jana Jumamosi limeua takriban watu 19, wakati Ijumaa jioni, kwa uchache watu 14 wa familia moja waliuawa katika shambulio la anga huko Darfur.
Mashambulizi hayo ambayo ni sehemu ya vita vinavyoendelea kati ya RSF na Jeshi la Sudan (SAF) tangu mwaka 2023 - yanaendelea baada ya siku sita mfululizo za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za kundi hilo dhidi ya Port Sudan ambao jeshi la Sudan limeufanya kuwa mji mkuu wake wakati huu wa vita.
Mapigano baina ya makundi hayo mawili yameharibu miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na gridi ya umeme na uwanja wa ndege wa mwisho wa kiraia uliokuwa unafanya kazi nchini humo. Uwanja wa Ndege wa mji wa Port Sudan ndio uliokuwa lango kuu la kuingizia bidhaa na mahitaji mbalimbali lililokuwa linatumiwa na Jeshi la Sudan.
Vita hivyo vimeshasababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa, watu milioni 13 kulazimika kuyahama makazi yao na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.
Kwa mujibu wa AFP, shambulio la jana Jumamosi dhidi ya gereza hilo limejeruhi pia watu 45. Usiku wa kuamkia jana pia watu 14 waliuawa katika kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk karibu na El-Fasher huko Darfur. Serikali ya Sudan inailaumu RSF kwa kufanya shambulio hilo.