Ghana: Afrika ipo tayari kushirikiana na Russia kuunda mustakabali wa kimataifa
Mbunge wa Ghana amesema Afrika iko tayari kuwa nguvu muhimu katika maendeleo ya kimataifa, akikaribisha uhusiano unaozidi kustawi wa bara hilo na Russia, alioutaja kama njia ya maendeleo endelevu.
Emmanuel Kwasi Bedzrah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ya Bunge ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi, aliyasema hayo katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Ushirikiano wa Kibinadamu wa Russia na Afrika katika Bunge la Russia (Duma) mjini Moscow.
Ameeleza bayana kuwa, "Nina imani ya dhati kwamba Afrika itatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya siku za usoni ya ubinadamu katika karne hii, na watu wake watafurahi kutembea njia ya maendeleo endelevu bega kwa bega na watu wa kimataifa wa Russia."
Haya yanajiri siku chache baada ya Russia kusema kuwa, serikali nyingi za Kiafrika zimedumisha msimamo huru, uliojikita katika kutoingilia kati masuala ya nchi nyingine, kuheshimu mamlaka ya kujitawala na uhuru wa kitaifa, na zimekataa kupasisha vikwazo dhidi ya Russia licha ya mashinikizo makubwa kutoka kwa nchi za Magharibi.
Tatyana Dovgalenko, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema hayo karibuni na kuongeza kuwa, nchi za Afrika zimeonyesha uelewa wa wazi wa sababu za mgogoro wa Ukraine na nafasi ya mataifa ya Magharibi katika kuuchochea.