Umoja wa Mataifa: Maafisa wetu wamezuiwa na M23 kuingia mashariki ya Congo
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wataalamu wake walizuiwa na waasi wa M23 kufanya uchunguzi wao katika ngome wanazoshikilia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa yake kwamba, maafisa wake walizuiliwa kufika katika miji inayokailiwa na waasi wa M23, kukusanya ushahidi kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa na waasi hao nchini Congo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNHCHR) hatua hiyo imezuia maafisa wake kutekeleza wajibu wao. Msemaji wa UNHCHR, Liz Throssell, amesema wataalamu hao wa UN walinyimwa vibali vya kuingia DRC na maafisa wa uhamiaji wa M23 katika eneo la mpakani la Gisenyi na Goma, licha ya kwamba maafisa hao walikuwa wamearifiwa mapema.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa baada ya kundi la M23 na serikali ya Congo kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki ya nchi. Wawakilishi wa pande zote mbili walitia saini tamko hilo Jumamosi iliyopita, kufuatia wiki kadhaa za mazungumzo ya kidiplomasia yaliyokuwa na lengo la kupunguza ghasia na taharuki mashariki mwa nchi hiyo.
Makubaliano hayo yanakuja wiki chache tu baada ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaini makubaliano ya amani mnamo Juni 27, na kuhuisha matumaini ya kumalizika kwa mapigano.
Maelfu ya raia wa DRC, nchi tajiri kwenye madini ya dhahabu na coltan, wanadaiwa kuuawa wakati kundi la M23, lilipokuwa likiendesha oparesheni ya kudhibiti miji ya Goma na Bukavu, mapema mwaka huu, na wataalamu wa Umoja wa Mataifa walilenga kukusanya ushahidi kuhusiana na suala hilo.