Uganda inawahifadhi wakimbizi karibu milioni mbili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129178-uganda_inawahifadhi_wakimbizi_karibu_milioni_mbili
Uganda inakaribia kuwa na wakimbizi milioni 2 huku machafuko yakiongezeka huko Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo mamia ya watu wanalazimika kuvuka mpaka kila siku na kuingia Uganda wakikimbia mapigano.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 05, 2025 11:04 UTC
  • Uganda inawahifadhi wakimbizi karibu milioni mbili

Uganda inakaribia kuwa na wakimbizi milioni 2 huku machafuko yakiongezeka huko Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo mamia ya watu wanalazimika kuvuka mpaka kila siku na kuingia Uganda wakikimbia mapigano.

Idadi kubwa ya wakimbizi wanayaacha makazi yao na kukimbilia kwenye maeneo salama nchini Uganda, huku kupunguzwa kwa misaada ya wafadhili kukiibua changamoto katika upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi hao. 

Bi Hamid Ibrahim Amin mkimbizi kutoka Sudan aliyewasili hivi karibuni nchini Uganda anasema: "Tulikuwa tunaishi Khartoum Sudan, lakini tulilazimika kuhamia Darfur kwa sababu ya vita. Hapa niko pamoja na mabinti zangu; mume wangu aliaga dunia. Hatuna chochote, hatuna pesa na hali ni ngumu sana". 

Tangu kuanza mwaka huu wa 2025, wastani wa watu 600 kwa siku wanawasili Uganda huku idadi ya wakimbizi kutoka Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo ikitarajiwa kufikia milioni 2 hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limeeleza kuwa: Uganda ambayo ni nchi inayohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika hivi sasa imepokea wakimbizi milioni moja na laki tisa ambapo wakimbizi zaidi ya milioni moja wana umri chini ya miaka 18.