Mgomo wa madaktari Kenya wakaribia, muungano wake watoa siku 14 kwa serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129254-mgomo_wa_madaktari_kenya_wakaribia_muungano_wake_watoa_siku_14_kwa_serikali
Sekta ya huduma za afya nchini Kenya, kwa mara nyingine inakabiliwa na mzozo baada ya Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) kutoa notisi ya siku 14 ya mgomo kutokana na kile inachosema kutotiliwa maanani kwa makubaliano waliyotiliana saini kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.
(last modified 2025-08-07T08:26:24+00:00 )
Aug 07, 2025 08:26 UTC
  • Mgomo wa madaktari Kenya wakaribia, muungano wake watoa siku 14 kwa serikali

Sekta ya huduma za afya nchini Kenya, kwa mara nyingine inakabiliwa na mzozo baada ya Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) kutoa notisi ya siku 14 ya mgomo kutokana na kile inachosema kutotiliwa maanani kwa makubaliano waliyotiliana saini kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Katika barua yao iliyotumwa kwa maafisa wakuu wa serikali, akiwemo Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei na Waziri wa Afya Aden Duale, Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah, ameishutumu serikali kwa kutoheshimu Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja wa 2017–2021 na maboresho yake.

Muungano huo umeeleza kuwa, serikali imeshindwa kutoa ruzuku za masharti kwa kaunti, kucheleweshwa kwa marekebisho ya mishahara, na kutolipa malimbikizo yaliyokubaliwa katika Mfumo wa Kurejea Kazini uliotiwa saini Mei 8, 2024.

Endapo madaktari hao watagoma, hatua hiyo italemaza huduma katika hospitali zote za umma nchi nzima ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.

Rais William Ruto wa Kenya

Mgomo wa mwisho wa madaktari nchi nzima nchini Kenya, uliomalizika Mei 8, 2024, ulichukua siku 56 na kutatiza pakuubwa huduma kwa maelfu ya raia.

Katika upande mwingine, Rais William Ruto wa Kenya ameikemea vikali serikali ya Marekani kufuatia mpango wake wa kuchunguza uhusiano wa Kenya na China, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kibiashara na taifa hilo la Asia ni kwa maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Rais Ruto amesema kwamba Kenya haipaswi kulaumiwa kwa kutafuta masoko mapya ya bidhaa zake, washirika wapya wa biashara na rasilmali, hasa katika ulimwengu unaoshuhudia mvutano wa kijiografia kati ya Amerika na China.