Jeshi la Sudan lawaua wapiganaji 40 mamluki wa Colombia
Jeshi la anga la Sudan limetangaza kuwa, limeiharibu ndege ya Imarati iliyokuwa imewabeba wapiganaji mamluki wa Colombia wakati ilipokuwa ikitua katika uwanja wa ndege unaodhibitiwa na jeshi huko Darfur, na kuwaua watu wapatao 40.
Hayo yameripotiwa na televisheni ya taifa inayoegemea upande wa jeshi. Duru ya jeshi imeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwa masharti ya kutotajwa majina kwamba ndege hiyo ya Umoja wa Falme za Kiarabu ilishambuliwa kwa bomu na kuharibiwa kabisa katika uwanja wa ndege wa Nyala huko Darfur.
Katika siku za hivi karibuni uwanja huo umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara kutokea angani na jeshi la Sudan linalopambana na na wapiganaji wanamgambo wa Rapid Support Forces, RSF, tangu Aprili 2023.
Hadi sasa hakuna kauli yoyoye iliyotolewa mara moja na RSF ama Umoja wa Falme za Kiarabu. Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Rais wa Baraza la Uongozi wa Mpito nchini Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kurudia ahadi yake aliyotoa ya kuvishinda na kuviondoa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika mkoa wa Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.
Mnamo tarehe 7 Juni 2024, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitangaza kuwa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF vilifanya "mauaji ya halaiki" katika kijiji cha Wad al-Noura kwa kuua wakazi 180 wa kijiji hicho. Mara nyingi RSF hukana kuhusika na mauaji ya raia.