Umoja wa Mataifa: Kundi la M23 liliua watu 319 DRC mwezi Julai
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, waasi wa M23 waliua watu zaidi ya 300 katika mwezi uliopita wa Julai katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amelikosoa kwa matamshi makali kundi la waasi wa M23 linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mauaji ya takriban watu 319 mashariki mwa DRC mwezi Julai.
Ofisi hiyo ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, imerekodi mashambulio mengi katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, na kwamba ipo haja ya kukomeshwa mashambulizi yote dhidi ya raia na kuwajibishwa kwa wale wote waliohusika.
Machafuko ya mwezi uliopita yametokea wiki chache baada ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M23 kutia saini tamko la pamoja mnamo Juni 19 mjini Doha, Qatar na kuthibitisha dhamira yao ya kusitisha mapigano ya kudumu.
Hata hivyo, licha ya kusainiwa kwa mikataba mingi ya usitishaji mapigano na mapatano, lakini bado nchi hiyo imeshuhudia kuvunjwa kwa makubaliano hayo na kushindwa kumaliza mizozo ya ndani iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kundi la waasi wa M23, ambalo linadhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limetishia kususia mchakato wa amani unaoendelea sasa kutokana na suala la kuachiliwa kwa wafungwa jambo ambalo Kinshasa inachelewa kufanya. Makubaliano hayo yaliyotiwa saini mjini Doha chini ya upatanishi wa Qatar, yalipendekeza usitishaji mapigano mara moja.