Mabadiliko ya baraza la mawaziri DRC yawaingiza wapinzani serikalini
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amelifanyia mabadiliko baraza la mawaziri na kuwateua viongozi kadhaa wa upinzani, kwa mujibu wa amri zilizosomwa kwenye televisheni ya taifa.
Baraza jipya la mawaziri bado linaongozwa na Waziri Mkuu, Judith Suminwa Tuluka, na linajumuisha wajumbe 53.
Kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani Adolphe Muzito ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Bajeti.
Floribert Anzuluni, kiongozi wa chama kidogo cha upinzani, ameteuliwa Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda.
Kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri huko Congo DR kunafuatia mashauriano ya kisiasa mwanzoni mwa mwaka, ambayo yalifuatana na mzozo wa usalama mashariki mwa nchi.
Mikoa yenye utajiri wa madini muhimu kama vile dhahabu na coltan, mashariki mwa DRC imekumbwa na mapigano kati ya makundi hasimu yenye silaha na kuingiliwa na mataifa ya kigeni kwa zaidi ya miaka 30.
Baada ya miezi kadhaa ya mapatano legevu ya kusitisha mapigano, DRC na kundi la M23 hatimaye zilitia saini tamko la kusitisha vita mnamo Juni 19.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, mashambulizi mapya dhidi ya raia yaliyofanywa na M23 na makundi mengine ya waasi yaliua takriban raia 319 mwezi uliopita wa Julai.