Mahakama yaagiza mwili wa Edgar Lungu kurejeshwa Zambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129312-mahakama_yaagiza_mwili_wa_edgar_lungu_kurejeshwa_zambia
Mahakama ya Afrika Kusini imeamua kuwa, serikali ya Zambia inaweza kuurejesha nyumbani mwili wa rais wa zamani Edgar Lungu na kumfanyia mazishi ya kitaifa, licha ya upinzani wa familia yake.
(last modified 2025-08-08T23:00:23+00:00 )
Aug 08, 2025 23:00 UTC
  • Mahakama yaagiza mwili wa Edgar Lungu kurejeshwa Zambia

Mahakama ya Afrika Kusini imeamua kuwa, serikali ya Zambia inaweza kuurejesha nyumbani mwili wa rais wa zamani Edgar Lungu na kumfanyia mazishi ya kitaifa, licha ya upinzani wa familia yake.

Mahakama kuu ya Pretoria iliamua kuunga mkono taifa la Zambia, ambalo hapo awali lilikuwa limewasilisha ombi la kuzuia mipango ya familia ya kumzika kwa siri nchini Afrika Kusini, ambako alifariki mwezi Juni.

Wakati huo, mawakili wa serikali ya Zambia walisema kuwa matakwa ya kibinafsi hayapaswi kupindua maslahi makubwa ya umma.

Mvutano huo unafuatia mzozo wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema, huku familia ya Lungu ikisema kuwa Hichilema ameonyesha kuwa hapaswi kuhudhuria mazishi yake.

Akitoa uamuzi huo, jaji Aubrey Ledwaba alisema serikali ya Zambia "ina haki ya kurejesha mwili wa marehemu rais" na akaamuru familia yake "kuusalimisha" mara moja kwa mamlaka.

Kufuatia kifo cha Lungu kutokana na ugonjwa ambao haujafahamika akiwa na umri wa miaka 68, familia ilitaka kusimamia taratibu za mazishi ikiwa ni pamoja na kurudisha mwili wake nyumbani, lakini mamlaka za Zambia zilitaka kudhibiti.

Lungu aliiongoza Zambia kuanzia 2015 hadi 2021 aliposhindwa katika uchaguzi na Hichilema kwa kura nyingi.

Baada ya kushindwa huko alijiondoa katika siasa lakini baadaye akarejea kwenye kinyang’anyiro hicho.