WHO: Karibu visa 100,000 vya kipindupindu vimeripotiwa Sudan
Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema visa karibu 100,000 vya maambukizi ya kipindupindu vimeripotiwa nchini Sudan tangu mwezi Julai mwaka uliopita huku likitahadharisha kuhusu njaa zaidi, watu kulazimika kuyakimbia makazi yao na milipuko zaidi ya magonjwa kutokea.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa, machafuko yasiyokoma yamesababisha baa la njaa, magonjwa na mateso, huku ugonjwa wa kipindupindu ukienea kote Sudan na majimbo yote yakiripoti mlipuko.
Ghebreyesus ameuambia mkutano wa waandishi habari wa chama cha waandishi habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva uliofanyika mjini Khartoum kwamba, kampeni za utoaji chanjo dhidi ya kipindupindu zilifanyika katika majimbo kadhaa ukiwemo mji mkuu Khartoum.
Wakati huo huo, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa, watu 80 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na zaidi ya maambukizi mapya 2,100 yamerekodiwa katika majimbo matano ya Darfur, nchini Sudan hadi kufikia Julai 30.
Katika taarifa yake, UNICEF imesema, kuanzia Juni 21 watu 20 walipoteza maisha kutokana na mripuko wa kipindupindu huku kesi 1,180 zikiripotiwa huko Tawila, katika Jimbo la Darfur Kaskazini.
Taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa UN imefafanua kuwa, hadi kufikia Julai 30 idadi ya wagonjwa wa kipindupindu katika majimbo matano ya Darfur imefikia karibu 2,140 na vifo visivyopungua 80 vimeripotiwa.