Kenya yasema marufuku ya Tanzania haitavuruga uhusiano
Serikali ya Kenya imetangaza kuwa, haina nia yoyote ya kulipiza kisasi dhidi ya Tanzania kufuatia uamuzi wake wa hivi majuzi wa kuwapiga marufuku wageni kushiriki katika biashara ndogo ndogo nchini humo.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Ujumuishaji wa Kikanda, Musalia Mudavadi Kinara wa Mawaziri wa Kenya alieleza kuwa mazungumzo ndiyo njia bora na endelevu zaidi ya kutatua migogoro ya kikanda.
Aidha aliongeza kusema kuwa Kenya haina mzozo wa kidiplomasia na taifa lolote na kwamba serikali imejitolea kuutatua mzozo huu kupitia mazungumzo na kuheshimiana.
Aliwahakikishia wajumbe wa kamati na umma kwa ujumla kuwa, serikali imejitolea kikamilifu kushirikiana kwa njia ya kujenga na mataifa jirani ili kulinda amani, kuimarisha ushirikiano, na kuhakikisha uthabiti wa muda mrefu wa eneo hili unabakia.
Wakati huo huo Waziri wa Ustawi wa Afrika Mashariki nchini Kenya, Wycliffe Oparanya, akizungumza kwenye maonyesho ya Bisahara ya Afrika Mashariki jijini Nairobi amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Tanzania vinahujumu biashara miongoni mwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Siku chache zilizpota Tanzania ilitoa agizo la kukataza wageni kujihusisha na biashara katika sekta 15 zikiwemo za uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, uongozaji watalii, uchimbaji mdogo wa madini, ununuzi wa mazao shambani, saluni za urembo, maduka ya bidhaa za kiutamaduni, pamoja na kuanzisha redio na televisheni.
Kulingana na taarifa za hivi karibuni, thamani ya biashara ya pande mbili kati ya Kenya na Tanzania kwa sasa inakadiriwa kufikia takribani Dola za Marekani milioni 900 - sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 140 za Kenya au Shilingi trilioni 2.3 za Tanzania kulingana na viwango vya ubadilishaji.