Kadhaa wajeruhiwa, biashara za mamilioni zachomwa moto katika machafuko ya Embu, Kenya
Kikosi maalumu cha wapelelezi kimetumwa mjini Siakago, Kaunti ya Embu nchini Kenya kufuatia wimbi la machafuko ambavyo yamesababisha wakazi kadhaa kujeruhiwa na mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kuharibiwa.
Machafuko hayo yalizuka wakati wafanyabiashara wa Meru na Embu walipokabiliana vikali mjini humo kwa sababu za uhasama wa kibiashara.
Kwenye ghasia hizo, majengo ya biashara, magari na mali nyinginezo ziliteketezwa.
Taharuki ilitanda huku makundi hayo mawili hasimu yakipigana na kusitisha biashara kwa siku mbili katika mji ambao kwa kawaida huwa wenye shughuli nyingi.
Waziri wa Huduma za Umma, Geoffrey Ruku, ametangaza kuwa makachero wanatazamiwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli kuhusu tukio hilo.
Ruku amewahakikishia wakazi kwamba wahusika wote wa machafuko hayo watawajibika akionya watumishi wa umma wakiwemo maafisa wa polisi ambao huenda walihusika na machafuko hayo.
“Hakuna atakayenusurika. Afisa yeyote atakayepatikana kuwa alisaidia au kupuuza maovu haya ataadhibiwa kikamilifu kisheria,” amesisitiza waziri huyo.
Wafanyabiashara kadhaa wamesimulia hasara walizopata kwenye ghasia hizo na kuwashutumu polisi kwa luacha kuwalinda.
Wafanyabiashara wa Meru wamekuwa wakiendesha biashara zao mjini humo na wakazi wamewashutumu kwa kuchukua biashara zao ikiwemo za Muguka.
Gavana wa Meru Mutuma M’Ethingia amekemea machafuko hayo akisema Wameru ni watu wanaojituma na wana haki kikatiba kufanya biashara, kumiliki mali, na kuishi sehemu yoyote ya Kenya bila ya kuingiliwa…/