Zaidi ya watu milioni nne wanakabiliwa na baa la njaa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129566-zaidi_ya_watu_milioni_nne_wanakabiliwa_na_baa_la_njaa_somalia
Idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa nchini Somalia inazidi kuongezeka katika nchi hiyo inayokabiliwa na ukosefu wa amani kutokana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 15, 2025 07:21 UTC
  • Watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano wapatao milioni 1.7 nchini Somalia wameathiriwa na utapiamlo kwa kukosa chakula.
    Watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano wapatao milioni 1.7 nchini Somalia wameathiriwa na utapiamlo kwa kukosa chakula.

Idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa nchini Somalia inazidi kuongezeka katika nchi hiyo inayokabiliwa na ukosefu wa amani kutokana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab.

Watu zaidi ya milioni nne nchini Somalia, wanakabiliwa na baa la njaa, huku wengine zaidi ya 100,000, wakiyakimbia makaazi yao kwa sababu ya ukosefu wa usalama tangu mwezi Juni mwaka huu.

Idara ya serikali inayoshughulikia masuala ya dharura nchini Somalia, imesema katika ripoti yake kwamba, kuna changamoto kubwa ya chakula ambayo imeanza kushuhudiwa tangu mapema mwaka huu, na hali imeendelea kuwa mbaya na kuongezeka kwa asilimia 29.

Idara ya serikali inayoshughulikia masuala ya dharura nchini Somalia imetangaza kuwa, inahitaji msaada wa dola 700,000 kukabiliana na hali hiyo.

Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukame mkubwa

 

Hali hii imesbabisha watu zaidi ya milioni nne kukabiliwa na njaa huku wengine zaidi ya milioni 2.5 wakiwa pia katika hatari ya kukosa chakula katika wilaya 26.

Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano wapatao Milioni 1.7 wameathiriwa pia na utapiamlo kwa kukosa chakula, huku maisha ya wengine 466,000 yakiwa katika hatari.

Haya yanajiri wakati huu, jimbo la Jubaland likiendelea kushuhudia ukosefu wa usalama, ambapo watu zaidi ya 38,000 wameyakimbia makaazi yao, wakiwemo zaidi ya 10,000 ambao wamevuka mpaka na kuingia katika nchi jirani ya Kenya.

Kundi la kigaidi la Al Shabab, ambalo lina mfungamano na mtandao wa Al Qaeda limekuwa likisababisha hofu kubwa nchini Somalia kwa zaidi ya miaka 16 sasa, na mara kwa mara hulenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali na raia wa nchi hiyo.