Kenya yalaumiwa kwa kupuuza ripoti ya dhulma kwa watoto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129608-kenya_yalaumiwa_kwa_kupuuza_ripoti_ya_dhulma_kwa_watoto
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International, limemshtumu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen kwa kupuuza uchunguzi uliofanywa na shirika moja kuhusu ulanguzi wa watoto nchini humo.
(last modified 2025-08-16T07:47:40+00:00 )
Aug 16, 2025 07:47 UTC
  • Kenya yalaumiwa kwa kupuuza ripoti ya dhulma kwa watoto

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International, limemshtumu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen kwa kupuuza uchunguzi uliofanywa na shirika moja kuhusu ulanguzi wa watoto nchini humo.

Akiwa mbele ya bunge hivi karibuni, Murkomen aliwaambia wabunge kwamba uchunguzi wa polisi uligundua kuwa ripoti ya shirika hilo la utangazaji la utangazaji la BBC ni ya uongo kwa sababu waliohojiwa walikuwa watu wazima.

Spika wa Bunge Moses Wetangula, pia aliishtumu makala hiyo na kusema ililenga kuiharibia nchi sifa.

Hata hivyo mkurugenzi wa shirika hilo la Amnesty nchini Kenya Irungu Houghton, amekanusha madai hayo na kusema, matamshi ya waziri huyo yaliwatia moyo wahusika wa biashara ya ngono kwa watoto na kuongeza kuwa ni jaribio la hatari la kudhalilisha na kunyamazisha uandishi wa habari.

Aprili mwaka huu ilitangazwa habari ya kuongezeka visa vya dhulma dhidi ya watoto katika jimbo la Marsabit, Kenya kwa kile kilichohusishwa na ufukara. Idadi kubwa ya wafugaji huwaoza mabinti zao kama njia ya kupata mifugo na mali ya kulea familia zao.

Umaskini na mila zilizopitwa na wakati zimetajwa kuchangia ongezeko la visa vya dhulma dhidi ya watoto wa kike katika jimbo la Marsabit. Familia nyingi za wafugaji huwaoza mabinti katika umri mdogo kama sehemu ya kupata chakula kwa familia na kuendeleza ufugaji.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mamlaka ya kukabiliana na majanga NDMA jimbo la Marsabit Guyo Golicha, athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababisha maafa kwa mifugo, pia imechangia hali hiyo kushuhudiwa.