Tanzania, Burundi zazindua ujenzi wa reli ya SGR Uvinza-Musongati
-
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na Rais wa Burundi, Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye wakizundua ujenzi wa reli ya kisasa ya Uvinza-Musongati
Mataifa mawili Jirani ya Tanzania na Burundi yamezindua ujenzi wa reli ya SGR Uvinza-Musongati.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Agosti 16, 2025) alishiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Uvinza hadi Musongati na kuwahahikishia Watanzania na WanaBurundi kwamba ujenzi huo utaanza katika muda uliopangwa.
Waziri Mkuu ambaye ameshiriki hafla hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema reli hiyo itakayokuwa na urefu wa km.240 pindi ikikamilika, itakuwa ndiyo reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika eneo la Musongati, Burundi, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutasaidia kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli.
“Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza,” alisema.
Mapema, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa alisema, utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na Ajenda 63 ya Umoja wa Afrika ambayo inataka bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa reli ya kisasa.
Alisema mbali na kuziunganisha nchi hizo mbili, kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo, kutarahisisha kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo.