Jeshi la Sudan latuhumiwa kuwatesa watu hadi kufa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129684-jeshi_la_sudan_latuhumiwa_kuwatesa_watu_hadi_kufa
Shirika maarufu la kutetea haki za binadamu nchini Sudan limelishutumu jeshi la nchi hiyo na vikosi vya usalama kwa kuwatesa watu hadi kuwaua pamoja na kuwa na "vyumba vya kufanya mauaji".
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 18, 2025 07:42 UTC
  • Jeshi la Sudan latuhumiwa kuwatesa watu hadi kufa

Shirika maarufu la kutetea haki za binadamu nchini Sudan limelishutumu jeshi la nchi hiyo na vikosi vya usalama kwa kuwatesa watu hadi kuwaua pamoja na kuwa na "vyumba vya kufanya mauaji".

Kundi la Wanasheria wa Dharura lilisema lina taarifa za mamia ya watu waliokamatwa katika mji mkuu Khartoum.

Adha taarifa hiyo inasema kuwa, katika hali mbaya zaidi, baadhi ya walioshikiliwa baadaye walipatikana wakiwa wamekufa na ushahidi unaonyesha waliteswa.

Jeshi la Sudan liliuteka tena mji huo kutoka kwa wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF) mnamo mwezi Machi, ambapo wanapigana vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimeua makumi ya maelfu katika kipindi cha miaka miwili.

Hayo yannajiri katika hali ambayo, mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa, wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) wamefyatua makombora kwenye kambi ya wakimbizi waliokumbwa na njaa katika eneo la magharibi mwa Darfur na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 31 wakiwemo watoto saba na mwanamke mjamzito.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilianza Aprili 2023 kutokana na mvutano wa kuwania madaraka kati ya makamanda wa jeshi na wa RSF. Mapigano hayo yameiharibu nchi hiyo ya Afrika, yamewalazimisha watu wapatao milioni 14 kuyahama makazi yao na kusababisha baadhi ya maeneo kukumbwa na baa la njaa.