Human Rights Watch yakosoa mpango wa Marekani wa kuiuzia Nigeria silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129738-human_rights_watch_yakosoa_mpango_wa_marekani_wa_kuiuzia_nigeria_silaha
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeikosoa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kuidhinisha mpango mpya wa mauzo ya silaha wa dola milioni 346 kwa Nigeria, likisema kuwa hatua hiyo inapuuza rekodi ya jeshi la Nigeria ya kile ilichokiita "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu."
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 19, 2025 23:47 UTC
  • Human Rights Watch yakosoa mpango wa Marekani wa kuiuzia Nigeria silaha

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeikosoa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kuidhinisha mpango mpya wa mauzo ya silaha wa dola milioni 346 kwa Nigeria, likisema kuwa hatua hiyo inapuuza rekodi ya jeshi la Nigeria ya kile ilichokiita "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu."

Shirika hilo lilisema jana Jumanne, kupitia mtafiti wake wa Afrika, Anietie Ewang, kwamba tangazo la mpango huo lililotolewa Alkhamisi iliyopita halikuzingatia dhamana yoyote ya uwajibikaji na kuzuia ukiukaji zaidi wa haki za binadamu.

Makubaliano hayo yanajumuisha risasi, makombora, mabomu na vifaa vingine vya kijeshi, na yanafuatia makubaliano ya awali ya dola milioni 997 yaliyoidhinishwa mwaka 2022 ya mauzo ya helikopta 12 za mashambulizi aina ya AH-1Z.

Human Rights Watch imesisitiza kuwa wasiwasi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Nigeria ni wa kweli na mpana. 

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema, katika kukabiliana na vitisho vya makundi kama Boko Haram, vikosi vya usalama vya Nigeria "vimejihusisha mara kwa mara katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, kuwekwa watu kizuizini kiholela, mateso na kadhalika."

Wakati huo huo, Mkuu wa Majeshi ya Nigeria, Jenerali Christopher Musa, ametetea utendakazi wa vikosi vya jeshi la nchi hiyo licha ya ukosoaji unaoongezeka wa ukiukwaji wa haki za binadamu, akisema kwamba jeshi la Nigeria wakati mwingine hulazimika kusitisha operesheni zake ili kulinda maisha ya raia.