Ajali ya boti yaua watu wasiopungua 22 kaskazini magharibi mwa Nigeria
Watu wasiopungua 22 wanaaminika kuwa wameaga dunia baada ya boti waliyokuwa wameabiri ndani yake kuzama kaskazini magharibi mwa Nigeria. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la huduma za dharura la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatano, boti hiyo ilikuwa imebeba wakulima 50 na wafanyabiashara waliokuwa wanaelekea kwenye soko ilipozama siku ya Jumapili katika jimbo la kaskazini magharibi la Sokoto.
Shirika la Taifa la Dharura (NEMA) limesema, Watu ishirini na tano waliokolewa muda mfupi baada ya ajali hiyo na wafanyakazi wa huduma za dharura na miili mitatu ilipatikana siku ya Jumanne.
Mkuu wa operesheni wa NEMA katika jimbo la Sokoto, Aliyu Kafindangi ameeleza kwamba, watu ishirini na mbili hawajulikani waliko huku juhudi za uokoaji zikiwa zimeshakamilika.
Kafindangi alivieleza vyombo vya habari hapo jana kwamba, shughuli za uokoaji zimesitishwa kwa sababu inaaminika kuwa baada ya saa 24, hakuna uwezekano wa kupatikana manusura.
Itakumbukwa kuwa, wakulima wasiopungua 16 walifariki katika ajali kama hiyo mwezi Agosti 2024 wakati boti yao iliyokuwa inawapeleka kwenye mashamba yao ya mpunga kuzama katika jimbo hilohilo la Sokoto.../