Raia 13 wauawa na wanamgambo wa RSF huko Darfur, Sudan
Raia wasiopungua 13 wa Sudan wameripotiwa kuuawa na wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) huko Darfur Kaskazini.
Wahanga hao ni pamoja na "watoto 5, wanawake 4, na wazee 4," Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao ya kijamii wa X.
Taarifa hiyo ya jana Jumapili ililielezea shambulio hilo katika eneo la Khazan Qolo katika barabara ya El-Fasher kuelekea Tawila kama "mauaji ya kuogofya" yaliyolenga raia.
Mtandao huo umeliita shambulio hilo "ukurasa mwingine katika kampeni inayoendelea ya maangamizi ya kizazi, na mauaji ya halaiki inayofanywa na RSF dhidi ya raia wasio na silaha huko Darfur, katika ukiukaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa na za kibinadamu."
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema, "Hujuma hii ya kimfumo dhidi ya watoto, wanawake, na wazee inathibitisha wazi kwamba, RSF inafuata sera ya makusudi ya kuwahamisha raia kutoka kwa ardhi yao kwa misingi ya kikabila."
Shambulio hili, mtandao huo umesema, "linajumuisha uhalifu kamili wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na linakinzana na wito wa RSF yenyewe kwa raia kuhama El-Fasher."
Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa, shambulizi la droni dhidi ya msafara wa maafisa wake umesababisha kuteketea kwa malori 16 ya misaada iliyokuwa inahitajika mno katika eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, lililokumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan SAF na RSF umepelekea kuzuka mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani na ambao unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku kutokana na juhudi za upatanishi kutozaa matunda.