Pigo jingine kwa Mpango wa Abraham; Kwa nini Libya inapinga uhusiano wa kawaida na Israel?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130014-pigo_jingine_kwa_mpango_wa_abraham_kwa_nini_libya_inapinga_uhusiano_wa_kawaida_na_israel
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imekataa nchi hiyo kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-08-26T12:03:23+00:00 )
Aug 26, 2025 12:03 UTC
  • Pigo jingine kwa Mpango wa Abraham; Kwa nini Libya inapinga uhusiano wa kawaida na Israel?

Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imekataa nchi hiyo kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abdul Hamid al-Dbeibeh, kuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, amekanusha madai kuwa nchi yake inajaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, akisema kuwa upinzani dhidi ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni suala lisilo na shaka miongoni mwa watu wa Libya. Ameongeza kuwa: "Madai kwamba tunakubali jinai ya kuwafukuza watu wa Palestina ni uwongo na uzushi wa vyombo vya habari."

Baadhi ya ripoti zimefichua mazungumzo ya siri kati ya maafisa wa Libya na Israel kuhusu kuwapa makazi Wapalestina kutoka Gaza, lakini serikali ya Libya imeyaita madai hayo "ya uchochezi na uongo kabisa" na kukanusha kuhusika na mipango hiyo.

Waziri Mkuu wa Libya alikuwa akiashiria baadhi ya ripoti kuhusu njama za Israel za kuwahamisha raia wa Gaza na kuwapeleka katika mataifa mengine ikiwemo Libya. Idhaa ya 12 ya Israel hivi karibuni ilidai kuwa baraza la mawaziri la Netanyahu lilikuwa katika mazungumzo na nchi tano za Indonesia, Somaliland, Uganda, Sudan Kusini na Libya ili kuwapokea wakaazi wa Gaza katika nchi hizo, lakini mtandao wa Kizayuni haukutaja matokeo ya mazungumzo hayo na iwapo yalikuwa hasi au chanya.

Habari hiyo inaripotiwa huku kukiwa na mipango ya Israel ya kuhimiza kile inachoeleza kuwa ni "uhamaji wa hiari" wa Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza hadi nchi nyingine, na kuibua wasiwasi wa haki za binadamu kuhusu kulazimishwa kwa Wagaza kuhama makazi yao kinyume na sheria za kimataifa.

Suala la kuhamishwa kwa nguvu watu wa Ukanda wa Gaza hadi nchi nyingine ni sera ambayo Israel imekuwa ikiitilia mkazo hasa katika miezi ya hivi karibuni.

Suala ambalo wakati mmoja lilizingatiwa kama njozi tu ya utaifa wa kupindukia wa utawala wa Kizayuni, sasa kutokana na vita vya Gaza na tangu Trump alipopendekeza kuwa ni suluhisho la mgogoro wa Gaza, wazo hili limebadilika taratibu kutoka kwenye uwanja wa fikra za utaifa na kuwa mkakati wa kiutendaji katika sera za Israel. Na hasa ikitiliwa maanani kuwa utawala wa Kizayuni unajaribu kuutekeleza kwa matumaini ya kubadilisha uwiano wa kisiasa na kidemografia katika eneo.

Ingawa mpango huu umepingwa tangu mwanzo na Wapalestina wanaoishi Gaza na vile vile nchi zinazoiunga mkono Palestina, nchi nyingi zinazozingatiwa na Trump na Netanyahu zimeukataa mpango huu na kusisitiza haki ya kisheria ya Wapalestina kubakia katika ardhi yao, ambapo mashirika mengi ya haki za binadamu yametangaza rasmi kwamba kuwalazimisha au kuwashinikiza Wapalestina waondoke nchini kwao kunaweza kuchukuliwa kuwa ni jinai ya kivita. Hata hivyo, utawala wa Kizayuni bado unasisitiza juu ya utekelezaji wa sera hiyo, na hivi sasa nchi za Kiafrika zinatizamwa kama sehemu zinazowezekana za kuwapokea wakimbizi wa Gaza.

Maandamano ya kupinga kuanzxishwa uhusiano wa kawaida na Israel

 

Bunge la Libya pia limepasisha kwa kauli moja kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kizayuni wa Israel ni uhalifu. Uamuzi huu unaonyesha unyeti mkubwa wa taasisi za kisiasa za Libya kwa suala hili. Kwa ujumla, msimamo wa Libya kuhusiana na suala la kluanzisha uhusiano wa kawaida na Israel umekuwa hasi kabisa na wa kupinga jambo hilo. Bunge la Libya hata lilitoa wito wa kusitishwa kwa usafirishaji wa mafuta kwa nchi zinazoiunga mkono Israel.

Anga ya kisiasa na kijamii nchini Libya ni mfuasi mkubwa wa Palestina, na jaribio lolote la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel hukabiliwa na hisia kali za ndani. Msimamo wa umma wa Libya kuhusu kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv ni mbaya na hilo linapingwa vikali. Upinzani huu hauonekani tu katika ngazi ya kisiasa bali pia miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii.

Mfano wa wazi ni tuukio la mwaka 2023 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Najla al Mangoush alilazimika kukimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi kwa kosa la kuonana na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini Italia. 

Katika kuonyesha hasira zao dhidi ya serikali baada ya waziri wa mambo ya nje wa Libya kuonana na waziri huyo Mzayuni, wananchi wenye hasira wa Libya waliechoma moto bendera ya Israel na kulaani kitendo chochote cha kuwa karibu na utawala katili wa Israel.

Upinzani dhidi ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel umekuwa ukishuuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiarabu

 

Pia, anga jumla ya umma nchini Libya inaunga mkono kwa dhati kadhia ya Palestina, na mawasiliano yoyote na Israel, hata katika ngazi ya kidiplomasia, yanakabiliwa na radiamali kali za kijamii.

Kiujumla Libya kwa muda mrefu imekuwa na misimamo dhidi ya Israel, haswa katika zama za kanali Muammar Gaddafi, na mtazamo huu umekuwa ni katika utamaduni wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Walibya wengi wanaiona Israeli kama "mvamizi" na wanaona maingiliano yoyote nayo kama ni usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Libya pia  wamechukua msimamo mkali dhidi ya kuanzishwa uhusiano wowote wa kawaida na Israel, wakitaka uwazi na uwajibikaji kutoka kwa serikali katika suala hili.

Wakati huo huo, jaribio lolote la kutaka kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Libya na Israel linaweza kuwa na madhara makubwa na kusababisha maandamano makubwa ya wananchi ndani ya nchi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Matokeo mengine ya hali hii ni kukithiri kwa msukosuko wa kisiasa, pamoja na uwezekano wa kusambaratika miungano ya kisiasa, kujiuzulu au kufukuzwa kazi kwa viongozi, na kuongezeka kwa migawanyiko kati ya makundi ya ndani. Hatua hiyo pia itapunguza uhalali wa serikali ya Libya.

Hasa kwa kuzingatia kwamba, sehemu kubwa ya watu na taasisi za kisiasa nchini Libya zinaipinga Israel, na hatua hiyo inaweza kutilia shaka uhalali wa serikali hiyo.

Suala jingine katika suala hili ni uhalifu wa kisheria. Katika suala hili, bunge la Libya kwa kauli moja lilipitisha sheria inayoharamisha kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel. Kwa hiyo, hatua yoyote katika uwanja huu inaweza kuwa na matokeo mabaya ya kisheria kwa viongozi.