Niger yalipiza kisasi, yaweka masharti magumu kwa wasafiri kutoka nchi za Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130118-niger_yalipiza_kisasi_yaweka_masharti_magumu_kwa_wasafiri_kutoka_nchi_za_ulaya
Kufuatia sheria mpya ya usafiri iliyowekwa na serikali ya Niger, raia wa nchi zilizoathirika sasa inawalazimu wawasilishe maombi yao ya visa katika balozi za Niger zilizoko Russia, Uswisi, na Uturuki.
(last modified 2025-08-28T11:34:11+00:00 )
Aug 28, 2025 11:34 UTC
  • Niger yalipiza kisasi, yaweka masharti magumu kwa wasafiri kutoka nchi za Ulaya

Kufuatia sheria mpya ya usafiri iliyowekwa na serikali ya Niger, raia wa nchi zilizoathirika sasa inawalazimu wawasilishe maombi yao ya visa katika balozi za Niger zilizoko Russia, Uswisi, na Uturuki.

Bakary Yaou Sangare, Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger, amenukuliwa akisema raia wa nchi hiyo wamekuwa wakikumbwa na “vikwazo” katika kupata visa za kuingia Ulaya tangu mapinduzi ya kijeshi nchini humo mnamo Julai 2023.

Waziri ameeleza kuwa raia wa Niger wamekuwa wakilazimika kusafiri hadi nchi jirani kwa ajili ya taratibu za visa, huku ombi la kutaka balozi za Ulaya zilizoko Niamey kutoa visa za kisheria likiwa halijajibiwa.

Sangare ameongeza kuwa: “Kuanzia sasa, balozi za Niger zilizoko Geneva, Ankara, na Moscow ndizo pekee zinazoruhusiwa kutoa visa za kuingia Niger kwa raia wa Italia, Uholanzi, Ujerumani, Ufalme wa Ubelgiji na Uingereza,”

Hata hivyo, ubalozi wa Niger mjini Brussels una “idhini ya kutoa visa kwa waombaji wenye paspoti za kidiplomasia na huduma,” ameongeza, akisisitiza kuwa hatua hizo zitatekelezwa vikali na haraka.

Ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey ulikuwa ukishughulikia utoaji wa visa za Schengen kwa raia wa Niger hadi mapinduzi ya kijeshi ya 2023, ambapo uhusiano kati ya Ufaransa na Niger ulianza kudorora, na kusababisha kufukuzwa kwa balozi wa Ufaransa.

Niger na washirika wake wa Sahel, Burkina Faso na Mali, wameilaumu Paris kwa kueneza uhasama na hivyo nchi zote tatu zimechukua hatua dhidi ya Ufaransa, ikiwemo kuvunja ushirikiano wa kijeshi.

Mnamo Desemba 2023, Niamey ilijitoa katika makubaliano mawili makubwa ya usalama na Umoja wa Ulaya na kufuta “kinga” zilizokuwa zimetolewa kwa vikosi vya Ulaya chini ya makubaliano hayo.

Jumatano, Shirika la Habari la Afrika liliripoti kuwa waziri wa mambo ya nje wa Niger amesema hatua mpya za visa kwa raia wa nchi zilizotajwa za Ulaya ni sehemu ya mageuzi ya kudhibiti uhamiaji na kulinda maslahi ya kitaifa huku mivutano ya kidiplomasia ikiongezeka.