Waafrika 1,700 wadaiwa kushiriki katika vita vya Russia, Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha amedai kwamba, zaidi ya Waafrika 1,700 wanapigana kwa niaba ya Russia katika vita vyake dhidi ya Ukraine, na kuongeza kwamba Moscow inatumia hadaa kuwasajili jeshini raia hao wa Kiafrika.
Akizungumza pamoja na mwenzake kutoka Ghana jijini Kiev jana Jumatano, Sybiha amesema kwamba majadiliano yanaendelea na serikali kote Afrika ili kuzuia raia wao kuvutiwa na mipango kama hiyo.
"Tunaona wazi kwamba Urusi inajaribu kuwavuta raia wa Afrika katika vita hatari," Sybiha ameambia mkutano na waandishi wa habari ma kuongeza kuwa, "Kulingana na data zetu, kwa sasa kuna zaidi ya raia 1,780 kutoka nchi 36 za bara la Afrika wanaopigana katika safu za jeshi la Russia."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa amesema kwamba Waafrika wengi wanaopigania Russia, walikuwa wahanga wa udanganyifu, wakivutiwa na mtandao fiche kwa ahadi ya kazi za kawaida. Amesema Ghana itashinikiza hatua kuchukuliwa kudhiibiti suala hilo wakati itakapokuwa mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika mwaka ujao.
Haya yanajiri siku chache baada ya Russia kukanusha madai kwamba inawaajiri Wakenya kupigana vitani nchini Ukraine, kufuatia ripoti za Huduma ya Kijasusi ya Kitaifa ya Kenya kwamba zaidi ya Wakenya 1,000 kwa sasa wanapigana upande wa Russia katika mzozo huo.
Ubalozi wa Russia umesema "unakanusha madai hayo kwa nguvu zote," ukiongeza kwamba mamlaka ya Russia "haijawahi kushiriki katika kuajiri raia wa Kenya kinyume cha sheria katika Vikosi vya Jeshi vya Shirikisho hilo."
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: Ubalozi wa Russia jijini Nairobi "haujatoa visa yoyote kwa Wakenya wanaotaka kusafiri hadi Russia kwa ajili ya kushiriki katika vita hivyo na umekanusha madia ya kuwahimiza kwa namna yoyote Wakenya kushiriki katika vita hivyo."