Watu 24 wauawa katika mashambulizi ya waasi wa RSF magharibi mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130124-watu_24_wauawa_katika_mashambulizi_ya_waasi_wa_rsf_magharibi_mwa_sudan
Watu wasiopungua 24 wameuawa na wengine 55 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya makombora ya waasi wa RSF katika mji mkuu wa El-Fasher, kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa Sudan.
(last modified 2025-08-28T11:45:15+00:00 )
Aug 28, 2025 11:45 UTC
  • Watu 24 wauawa katika mashambulizi ya waasi wa RSF magharibi mwa Sudan

Watu wasiopungua 24 wameuawa na wengine 55 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya makombora ya waasi wa RSF katika mji mkuu wa El-Fasher, kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa Sudan.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema katika taarifa mapema leo Alhamisi kuwa waasi wa RSF wamelenga soko kuu na mtaa wa Awlad Al-Reef katika mji wa El-Fasher, na kusababisha vifo vya watu 24 na majeruhi 55, wakiwemo wanawake 5.

Shirika hilo limesema: “Uhalifu huu wa kikatili ni mfululizo wa uhalifu wa kivita na vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasio na silaha katika mji wa El-Fasher kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku kukiwa na mzingiro mkali na upungufu mkubwa wa chakula, dawa na huduma muhimu."

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuwashinikiza vinara wa RSF wasitishe mauaji ya kimbari, njaa ya makusudi, mashambulizi ya makombora na mzingiro dhidi  wa mji El-Fasher.”

Mji wa El-Fasher umekuwa chini ya mzingiro tangu Mei, na mashirika ya ndani ya Sudan yanawalaumu waaasi wa RSF kwa kushambulia maeneo ya raia licha ya wito wa kimataifa wa kulinda miji.

Waasi wa RSF walianzisha uasi dhidi ya serikali Aprili 2023 na hadi sasa vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kusababisha wengine milioni 14, kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. Serikali ya Sudan inasema waasi wa RSF wanapata himaya ya kigeni hasa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Hata hivyo UAE imekanusha tuhuma za kuunga mkono waasi hao.