Makumi wauawa katika mashambulizi pacha ya magaidi Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137046-makumi_wauawa_katika_mashambulizi_pacha_ya_magaidi_nigeria
Watu wasiopungua 25 wameuawa huku nyumba kadhaa zikichomwa moto baada ya watu wenye silaha kushambulia vijiji viwili katika Jimbo la Adamawa, kaskazini mashariki mwa Nigeria usiku wa kuamkia jana.
(last modified 2026-02-26T09:13:16+00:00 )
Feb 26, 2026 05:10 UTC
  • Makumi wauawa katika mashambulizi pacha ya magaidi Nigeria

Watu wasiopungua 25 wameuawa huku nyumba kadhaa zikichomwa moto baada ya watu wenye silaha kushambulia vijiji viwili katika Jimbo la Adamawa, kaskazini mashariki mwa Nigeria usiku wa kuamkia jana.

Wabeba silaha hao walishambulia wakazi wa vijiji vya Kirchinga katika wilaya ya Madagali na Garaha katika wilaya jirani ya Hong, karibu na Msitu wa Sambisa ambapo magaidi wa Boko Haram na ISWAP wanaendesha harakati zao.

Abubakar Lawan Kanuri, Mkuu wa kijiji cha Kirchinga, aliiambia Reuters jana Jumatano kwamba, washambuliaji walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi ambayo mwanzoni yaliwafanya wakazi kudhania kuwa wanamgambo hao ni wanajeshi waliokuwa wanashika doria.

Kanuri amesema watu 18 waliuawa baada ya watu hao wenye silaha kujipenyeza katika jamii na kutekeleza ukatili huo wa kuogofya, sambamba na kuteketeza nyumba moto.

Huko Garaha, watu saba waliuawa wakati watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki zaidi ya 50 walipovamia kijiji hicho na kushambulia kambi ya kijeshi iliyoko karibu, amesema mkazi wa kijiji hicho Musa Isa, ambaye ameongeza kuwa "aliponea chupuchupu."

Haya yanajiri siku chache baada ya kundi moja la wabeba silaha kuwaua watu wasiopungua 50 na kuwateka nyara wanawake na watoto katika shambulio la usiku kwenye kijiji kimoja kilichoko katika Jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Nigeria yanaendelea kukabiliana na vitisho vya usalama vinavyoandamana, ikiwa ni pamoja na magenge ya wahalifu wenye silaha na wapiganaji wa makundi ya waasi.