Polisi Kenya wagundua miili zaidi ya waliouawa na pote la Kikristo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130156-polisi_kenya_wagundua_miili_zaidi_ya_waliouawa_na_pote_la_kikristo
Uchunguzi nchini Kenya kuhusu vifo vinavyoshukiwa kutekelezwa na wafuasi wa kikundi cha Kikristo chenye misimamo mikali katika kaunti ya Kilifi ulichukua mkondo wa kutisha siku ya Alhamisi, baada ya polisi kufukua miili mingine saba katika kijiji cha Kwa Binzaro.
(last modified 2025-08-29T10:48:22+00:00 )
Aug 29, 2025 10:48 UTC
  • Polisi Kenya wagundua miili zaidi ya waliouawa na pote la Kikristo

Uchunguzi nchini Kenya kuhusu vifo vinavyoshukiwa kutekelezwa na wafuasi wa kikundi cha Kikristo chenye misimamo mikali katika kaunti ya Kilifi ulichukua mkondo wa kutisha siku ya Alhamisi, baada ya polisi kufukua miili mingine saba katika kijiji cha Kwa Binzaro.

Maafisa wa polisi wamekusanya vipande 54 vya miili vilivyokuwa vimetawanyika katika eneo hilo.

Daktari wa serikali wa uchunguzi wa maiti, Richard Njoroge, aliyekuwepo katika eneo la tukio, amesema kuwa hali ya mabaki ya miili iliyopatikana inaashiria maziko ya hivi karibuni.

Dkt. Njoroge amesema: “Tumeona kuwa katika eneo hili, miili inaonekana kuwa bado mipya. Haijageuka kuwa mifupa pekee kama ile tuliyopata wiki iliyopita. Miili tuliyofukua wiki iliyopita ilikuwa mifupa tupu bila mabaki ya nyama, lakini hii tuliyoipata hapa inaonekana kuzikwa miezi michache au wiki chache zilizopita.”

Ugunduzi huu wa hivi karibuni unafuatia kufukuliwa kwa miili mingine mitano kutoka makaburi katika eneo hilo hilo mnamo Agosti 21, jambo linalozua hofu ya mauaji mengine yanayofanana na mkasa wa Shakahola wa mwaka 2023.

Mamlaka zimewahimiza jamaa wa watu waliopotea kufika katika dawati la Msalaba Mwekundu wa Kenya lililoko Hospitali ya Wilaya ya Malindi ili kuwasilisha taarifa binafsi na sampuli za DNA kwa ajili ya utambuzi wa miili.

Uchunguzi huu unafanana na mkasa wa mauaji ya msitu wa Shakahola, pia katika Kilifi, ambako miili ya zaidi ya waathiriwa 430 wa Kanisa la Good News International la kasisi Paul Mackenzie ilifukuliwa mwaka 2023.

Wengi walibainika kufariki kutokana na njaa, kukosa hewa na ukatili—tukio ambalo wachunguzi walilitaja kama ibada ya njaa yenye misimamo mikali ya Kikristo.

Kuna wasiwasi kuwa Mackenzie, ambaye yuko gerezani huku kesi yake ya mauaji ikiendelea, bado anaendesha shughuli zake za uhalifu na misimamo mikali akiwa gerezani, akishirikiana na baadhi ya maafisa wa usalama.

Kaunti ya Kilifi iko katika eneo la pwani, takriban kilomita 426 kusini mashariki mwa Nairobi.