Ripoti: Mripuko wa kipindupindu umeua watu 113 nchini Chad
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mripuko wa kipindupindu nchini Chad tangu mwezi Julai mwaka huu mpaka sasa imefikia 113.
Wizara ya Afya ya Chad imesema hayo katika taarifa yake na kuongeza kuwa, jumla ya kesi 1,631 zinazoshukiwa kuwa za maradhi hayo zimerekodiwa.
Taarifa hiyo imesema, takwimu hizo ziliripotiwa wakati wa mkutano ulioongozwa na Waziri wa Afya ya Umma, Abdelmadjid Abderahim kujadili mikakati ya kuzuia ugonjwa huo kuenea.
Wizara ya Afya ya Chad imesema nchi hiyo imepokea dozi 1,120,295 za chanjo ya kipindupindu, ikiongeza kuwa dozi hizo zinapelekwa katika eneo la mashariki kwa ajili ya kampeni ya chanjo.
Serikali imewataka wananchi wa Chad kudumisha usafi ili kusaidia kuzuia kuenea kwa maambukizi zaidi ya ugonjwa huo. Kisa cha kwanza cha kipindupindu kiligunduliwa katika kambi ya wakimbizi ya Dougui katika eneo la mashariki la Ouaddai mnamo Julai 13. Kambi hiyo inahifadhi takriban wakimbizi 20,000 wa Sudan.
Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) lilitahadharisha kuwa, watoto 80,000 wako katika hatari kubwa ya kupatwa na kipindupindu kufuatia kuanza kwa msimu wa mvua magharibi na katikati mwa Afrika.
Watoto, hususan wale wenye umri chini ya miaka mitano wako katika hatari ya kupata kipindupindu kutokana na sababu kama vile usafi duni, ukosefu wa vyoo na maji salama, na upo uwezekano mkubwa wa kupungukiwa na maji mwilini.