WHO yasikitishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya wahudumu wake Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128608-who_yasikitishwa_na_mashambulizi_ya_israel_dhidi_ya_wahudumu_wake_gaza
Jeshi la Israel lilishambulia mara tatu makazi ya wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Ukanda Gaza, pamoja na ghala lake kuu jana Jumatatu , amesema mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
(last modified 2025-10-17T05:53:46+00:00 )
Jul 22, 2025 04:24 UTC
  • WHO yasikitishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya wahudumu wake Gaza

Jeshi la Israel lilishambulia mara tatu makazi ya wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Ukanda Gaza, pamoja na ghala lake kuu jana Jumatatu , amesema mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika taarifa kwamba, mashambulizi hayo ya wanajeshi ya Israel yalilenga makazi ya wafanyikazi wa taasisi hiyo ya kimataifa huko Deir al Balah.

"Jeshi la Israel liliingia katika majengo hayo, na kuwalazimisha wanawake na watoto kuondoka kwa miguu kuelekea Al-Mawasi huku kukiwa na vita vikali," amesema Dakta Tedros.

Ameeleza bayana kuwa, wafanyakazi wa kiume na jamaa zao walifungwa pingu, kuvuliwa nguo, kuhojiwa papo hapo na kupekuliwa huku wakiwa wameelekezewa mtutu wa bunduki, na kuongeza kuwa wafanyakazi wawili wa WHO na wanafamilia wawili walikamatwa.

"Watatu waliachiliwa baadaye, lakini mfanyakazi mmoja bado yuko kizuizini," amesema Mkuu wa WHO na kuongeza kuwa, "WHO inataka kuachiliwa mara moja kwa mfanyakazi anayezuiliwa; na kuhakikishia ulinzi wa wafanyikazi wake wote."

Akieleza wasiwasi wake kuhusu amri ya hivi karibuni ya Israel ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina huko Deir al Balah, Tedros amesisitiza kwamba, agizo hilo limeathiri majengo kadhaa ya WHO, na kulemeza uwezo wa shirika hilo kufanya kazi huko Gaza, jambo ambalo limefanya mfumo wa afya wa Gaza uelemewa zaidi, na sasa unaelekea kuporomoka kikamilifu.