WHO: Chanjo ya Ebola yaanza kutolewa kusini mwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130830-who_chanjo_ya_ebola_yaanza_kutolewa_kusini_mwa_drc
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, utoaji chanjo kwa watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola umeanza kusini mwa jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
(last modified 2025-09-15T10:48:51+00:00 )
Sep 15, 2025 10:48 UTC
  • WHO: Chanjo ya Ebola yaanza kutolewa kusini mwa DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, utoaji chanjo kwa watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola umeanza kusini mwa jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Taarifa zinasema kuwa, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kutoa chanjo dhidi ya maambukizo mapya ya virusi vya Ebola, ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu 28 tangu Agosti 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO chanjo hiyo ilianza kuchomwa Jumapili ya wiki iliopita kwa zaidi ya raia 400, katika mji wa Bulape mkoani Kasai, chanjo hiyo ikitolewa kwa wale ambao tayari wameathirika na wahudumu wa afya.

Mlipuko wa ugonjwa huo hatari uliripotiwa mapema mwezi huu kwenye kitongoji cha Bulape na kusababisha vifo vya watu 16 na wengine 68 wanashukiwa kuwa wameambukizwa.

WHO imesema dozi za awali zipatazo 400 za chanjo aina ya Ervebo zimetolewa na shehena nyingine ya chanjo itapelekwa siku chache zinazokuja.

Miongoni mwa wanaopatiwa chanjo hizo ni maafisa wa afya walio mstari wa mbele na watu inaoaminika huenda watapata maambukizi kutokana na ukaribu wao na waliokwishaambukizwa.

Mara ya mwisho kwa maambukizo hayo kuripotiwa nchini DRC, ilikuwa miaka mitatu iliyopita ambapo watu 6 waliripotiwa kufariki. Jamhuuriy a Kidemokrasia ya Congo ikiwa na historia ya kusumbuliwa milipuko ya Ebola tangu mwaka 1976, ila kati ya mwaka 2018 hadi mwaka 2020 ndipo nchi hiyo imeshuhudia kipindi kirefu cha mlipuko wa ugonjwa huo zaidi ya watu 2, 300 wakiripotiwa kufa.