Eritrea yapuuzilia mbali madai ya Ethiopia ya kutaka kuanzisha vita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131804-eritrea_yapuuzilia_mbali_madai_ya_ethiopia_ya_kutaka_kuanzisha_vita
Eritrea imepuuzilia mbali shutuma zilizotolewa na Ethiopia kwamba nchi hiyo inajiandaa kuanzisha vita ikisema ni ''matamshi ya uchochezi''.
(last modified 2025-10-09T22:58:01+00:00 )
Oct 09, 2025 22:58 UTC
  • Eritrea yapuuzilia mbali madai ya Ethiopia ya kutaka kuanzisha vita

Eritrea imepuuzilia mbali shutuma zilizotolewa na Ethiopia kwamba nchi hiyo inajiandaa kuanzisha vita ikisema ni ''matamshi ya uchochezi''.

Gedion Timothewos Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia tarehe Pili mwezi huu wa Oktoba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo alidai kuwa, Eritrea imekuwa ikishirikiana na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF); kundi la upinzani lenye makazi yake huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Gebremeskel amesema kuwa barua hiyo ni ya ''udanganyifu''.

Yemane ameishutumu Ethiopia kwa kupanga njama za kuudhofisha ''uhuru wake uliopatikana kwa juhudi kubwa'' kwa kujaribu kujipatia nafasi ya kuifikia bandari yake.

Uhusiano kati ya nchi hizi mbili jirani umekuwa ukizorota pakubwa zaidi katika miezi ya hivi karibuni.

Itakumbukwa kuwa, Eritrea ilichukua udhibiti wa ukanda wa pwani wa Bahari Nyekundu ilipopata uhuru kutoka Ethiopia mwaka 1993.

Vita vya mpakani kati ya nchi mbili hizo kati ya mwaka 1998 na 2000 vilipelekea kuuawa makumi ya maelfu ya watu.

Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia alifanya jitihada ili kupunguza hali ya mvutano na nchi hiyo jirani alipoingia madarakani mwaka 2018. Hata hivyo katika miaka ya karibuni Ethiopia imekuwa ikifanya kila linalowezekana ili kuweza kuifikia Bahari Nyekundu hatua ambayo imesababisha kuzorota uhusiano wa nchi hiyo na jirani yake Eritrea.