Ajali ya basi yaua watu 42 nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131936-ajali_ya_basi_yaua_watu_42_nchini_afrika_kusini
Watu wasiopungua 42 wamepoteza maisha baada ya basi walilokuwa wakisafiria kubingiria katika jimbo la Limpopo, kaskazini mwa Afrika Kusini.
(last modified 2025-10-13T09:29:39+00:00 )
Oct 13, 2025 09:29 UTC
  • Ajali ya basi yaua watu 42 nchini Afrika Kusini

Watu wasiopungua 42 wamepoteza maisha baada ya basi walilokuwa wakisafiria kubingiria katika jimbo la Limpopo, kaskazini mwa Afrika Kusini.

"Waliofariki dunia ni pamoja na wanawake 18, wanaume 17 na watoto saba," Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini SABC limesema, likinukuu Wizara ya Uchukuzi ya nchi hiyo.

Harbari zaidi zinaeleza kuwa, zaidi ya abiria 30 wamelazwa hospitalini baada ya dereva wa basi hilo lililokuwa limebeba raia wa Malawi na Zimbabwe kushindwa kulidhibiti na kupelekea lianguke.

Wizara ya Uchukuzi ya Afrika Kusini imesema uchunguzi kuhusu ajali hiyo unaendelea, huku ikitoa rambirambi zake kwa familia za waliofariki dunia.

"Hili ni janga la kuhuzunisha," amesema Mkuu wa Mkoa wa Limpopo Phophi Ramathuba. "Kwa niaba ya serikali ya Mkoa wa Limpopo, tunatuma rambirambi zetu kwa familia zilizoathirika, ikiwa ni pamoja na zile za Zimbabwe na Malawi. Tunawatakia afueni ya haraka manusura wote."

Waliojeruhiwa wanaendelea kutibiwa hospitalini, huku serikali ya mkoa wa Limpopo ikisema huduma za kisaikolojia zinatolewa kwao.

Hivi karibuni pia, takriban watu 20 walipoteza maisha baada ya lori kugongana na basi lililokuwa likisafirisha wachimba migodi katika jimbo hilo la Limpopo.

Aidha Machi mwaka jana, watu wasiopungua 45 walifariki dunia nchini wakati basi lililokuwa limebeba wafanyaziara wa Pasaka kutumbukia kwenye daraja katika jimbo hilo hilo la kaskazini mashariki.