Afrika Kusini yalaani mpango wa wakimbizi wa Marekani kwa mapungufu yake mengi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132674-afrika_kusini_yalaani_mpango_wa_wakimbizi_wa_marekani_kwa_mapungufu_yake_mengi
Serikali ya Afrika Kusini imelezea kusikitishwa na mpango wa wakimbizi wa Marekani, ikiuelezea kuwa si sahihi ni upotoshaji na una mapungufu mengi.
(last modified 2025-11-01T11:40:16+00:00 )
Nov 01, 2025 11:40 UTC
  • Afrika Kusini yalaani mpango wa wakimbizi wa Marekani kwa mapungufu yake mengi

Serikali ya Afrika Kusini imelezea kusikitishwa na mpango wa wakimbizi wa Marekani, ikiuelezea kuwa si sahihi ni upotoshaji na una mapungufu mengi.

Matamshi hayo yametolewa na Afrika Kusini baada ya Marekani kutangaza kwamba imepanga kupokea wakimbizi 7,500, wengi wao wakiwa Waafrika Kusini Wazungu ambao Marekani inadai eti wameathiriwa na "mauaji ya kimbari."

Idara ya Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini (DIRCO) imelaani madai hayo ya uongo ya Marekani na kusema: "Madai ya kutokea 'mauaji ya kimbari ya wazungu' nchini Afrika Kusini hayana ushahidi wowote wa kutegemewa. Hii inathibitishwa zaidi na barua ya wazi na ya kizalendo kutoka kwa wanachama maarufu wa jamii ya Waafrikana wenyewe ambao wamepinga hadharani ngano hizo zisizo na ukweli za Marekani."

DIRCO ilisisitiza kwamba, kuna tofauti kati ya uhamiaji wa hiari na kuhamia nchi nyingine kama mkimbizi.

Taarifa hiyo pia imesema: "Mpango uliobuniwa na Marekani wa kurahisisha uhamiaji wao na kuelekea kwenye makazi mapya kama wakimbizi, kimsingi una upungufu mkubwa." 

Taarifa hiyo imebainisha pia kuwa Katiba ya Afrika Kusini inalinda kikamilifu haki ya raia yeyote na maamuzi yake ya kuhamia sehemu nyingine kwa njia za kisheria.

DIRCO imesisitiza zaidi kwamba ingawa ilifanya tathmini ya kina ya uhusiano wake na serikali ya Marekani na kuupa kipaumbele ushirikiano wa pande mbili na kutatua masuala tata ya pande zote kupitia mazungumzo na kuheshimiana kama zinavyosema sheria ya kimataifa na uhuru wa kitaifa, lakini Marekani inapotosha mambo na kwamba Afrika Kusini haikubaliani na upotoshaji kama huo.