RSF yawatia mbaroni wanamgambo wake wanaotuhumiwa kufanya jinai el Fasher Sudan
Vikosi vya Msaa wa Haraka RSF nchini Sudan vimetangaza kuwa vimewatia mbaroni wapiganaji wanaoshutumiwa kukiuka haki za binadamu na kufanya mauaji ya umati kwenye mji wa El-Fasher uliotekwa na kundi hilo hivi karibuni.
Video iliyosambazwa na kundi hilo kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram inamuonesha mpiganaji aliyetambuliwa kwa jina la Abu Lulu akiwekwa kizuizini katika kile RSF ilichodai kuwa ni gereza huko Darfur Kaskazini. Abu Lulu alikuwa ameonekana katika video za TikTok akifanya mauaji baada ya kutekwa mji wa El-Fasher.
Wakati RSF ilipochukua udhibiti wa mji huo uliokuwa umezingirwa kwa muda mrefu huko Darfur Kaskazini siku ya Jumapili, watu walioshuhudia wamesema kuwa kulizuka mauaji ya kutisha kutoka kwa wapiganaji wa RSF, mauaji ambayo inaonekana yamefanyika kikabila. Kiongozi mmoja wa RSF ambaye jina lake halikutajwa anaonekana kwenye video hiyo akisema kuwa, Abu Lulu amekamatwa kwa mujibu wa maagizo ya Kamanda Mkuu wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo.
El-Fasher ilizingirwa na RSF kwa zaidi ya siku 500 wakati kundi hilo lilipokuwa linapambana na jeshi la Sudan SAF mpaka lilipouteka mji huo ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini siku ya Jumapili.
Katika upande mwingine Mratibu wa Msaada wa Dharura wa Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama siku ya Alkhamisi kwamba kuna "ripoti za kuaminika za kufanyika mauaji makubwa huku raia wakiendelea kuukimbia mji wa El-Fasher.
Kuangukia mji wa El-Fasher mikononi mwa waasi kumezua hofu kwamba Sudan ambayo ni nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika inaweza kugawanyika vipande vipande huku RSF ikishikilia Darfur na jeshi likishikilia mji mkuu Khartoum na maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi.