Sudan Kusini: Hatutaegemea upande wowote katika mzozo wa Sudan
-
Luteni Jenerali Johnson Olony
Naibu Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Sudan Kusini, Luteni Jenerali Johnson Olony, amesema nchi yake haitaegemea upande wowote katika mzozo unaoendelea katika nchi jirani ya Sudan.
Luteni Jenerali Johnson Olony amesema hayo katika taarifa fupi akieleza kwamba vikosi vyake vitalinda eneo la Heglig na visima vyake vya mafuta katika jimbo la Kordofan Magharibi.
Jeshi la Sudan Kusini pia limeonyesha picha za wanajeshi wa Sudan wa Brigedi ya 90 ndani ya ardhi yake, baada ya kuondoka eneo la Heglig.
Picha hizo zinaonyesha vifaru, magari ya kivita, silaha nzito na risasi zilizokusanywa na wanajeshi wa Sudan Kusini, ili kuandaa mazingira ya kurudishwa wanajeshi wa Sudan nchini kwao.
Jumatatu wiki hii, wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) walitangaza kwamba wamechukua udhibiti wa uwanja wa mafuta wa Heglig, na kusisitiza kuwa "wanalinda mitambo muhimu ya mafuta katika eneo hilo kwa njia inayolinda maslahi ya Jamhuri ya Sudan Kusini, ambayo inategemea sana mtiririko wa mafuta kupitia eneo la Sudan hadi kwenye masoko ya kimataifa."
Jana Jumanne, vyanzo vya ndani viliripoti kwamba ndege isiyo na rubani isiyojulikana iliwalenga viongozi mashuhuri wa "Utawala wa Jimbo la Kordofan Magharibi" katika eneo la "Fama" karibu na uwanja wa mafuta wa Heglig, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.
Kwa upande wake, Muungano wa Waasisi wa Sudan, unaoongozwa na Kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, umesema kwamba viongozi saba wa utawala wa eneo hilo wameuawa wakati wa ziara yao Heglig kwa shambulio la ndege zisizo na rubani, wakilituhumu jeshi la Sudan kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Serikali ya Sudan haijatoa taarifa yoyote kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yake na RSF.