Waguinea Bissau waandamana kulaani mapinduzi, viongozi wa kanda wakutana kutafuta suluhisho
Mamia kadhaa ya watu wameingia barabarani katika mji mkuu wa Guinea-Bissau, Bissau kupinga mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita viongozi wa upinzani wanaoshikiliwa waachiliwe huru, huku viongozi wa kikanda wakijiandaa kukutana leo Jumapili kujadili namna ya kuupatia suluhisho mgogoro huo.
Waandamanaji hao walikabiliana na vikosi vya usalama mjini Bissau, wakichoma matairi na kupiga makelele ya kutaka Domingos Simoes Pereira, kiongozi wa Chama cha Afrika kwa ajili ya Uhuru wa Guinea-Bissau na Cabo Verde (PAIGC), aachiliwe huru.
Kwa mujibu wa jamaa zake na duru za usalama, Pereira alikamatwa wakati wa hekaheka za mapinduzi hayo ya kijeshi.
Maafisa wa jeshi waliamua kumwondoa madarakani Rais Umaro Sissoco Embalo tarehe 26 Novemba, siku moja kabla tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya uchaguzi wa bunge na urais. Siku iliyofuata, wanajeshi waliofanya mapinduzi walimteua Meja Jenali Horta Inta-a kuwa kiongozi wa mpito.
Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS leo watakutana Abuja, Nigeria, kujadili hali ya Guinea-Bissau na kuangalia uwezekano wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa kauli iliyotolewa wiki iliyopita na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone Timothy Musa Kabba.
"Hatutambui serikali ya mpito," alisema mwanaharakati wa asasi za kiraia Vigario Luis Balanta katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, akihimiza kufanyika mgomo wa kitaifa na wiki ya uasi wa sheria.
"Sisi ni vijana na sisi ni mustakabali wa nchi hii," alisisitiza mwanandamanaji Antonio Sami. "Hatutawahi kamwe kukubali kwamba uhuru wetu uhojiwe."
Siku ya Jumatano, uongozi wa kijeshi nchini Guinea Bisssa ulizindua hati ya mpito ya miezi 12 inayomzuia Inta-a na waziri wake mkuu kushiriki katika uchaguzi wa baadaye, ikitangaza ramani ya kazi wiki mbili baada ya kusimamisha katiba.
Mapinduzi ya Novemba ni ya tisa katika kanda ya Afrika Magharibi na Kati ndani ya miaka mitano na ni sehemu ya mfululizo wa hali ya kukosekana utulivu nchini Guinea-Bissau.../