Afrika yakosoa hatua ya Trump ya kuiondoa US katika taasisi za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135470-afrika_yakosoa_hatua_ya_trump_ya_kuiondoa_us_katika_taasisi_za_kimataifa
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mahmoud Ali Youssouf ametoa wito wa kuimarishwa mifumo ya pande nyingi ili kushughulikia changamoto za kimataifa, siku chache baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kujiondoa katika taasisi mbalimbali za kimataifa.
(last modified 2026-01-14T03:15:46+00:00 )
Jan 14, 2026 03:15 UTC
  • Afrika yakosoa hatua ya Trump ya kuiondoa US katika taasisi za kimataifa

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mahmoud Ali Youssouf ametoa wito wa kuimarishwa mifumo ya pande nyingi ili kushughulikia changamoto za kimataifa, siku chache baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kujiondoa katika taasisi mbalimbali za kimataifa.

AU imesema katika taarifa ya jana Jumanne kwamba, Mwenyekiti wa umoja huo amesikitishwa na dikri ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, ya kusitishwa ushiriki na ufadhili wa Washington kwa mashirika 66 ya Umoja wa Mataifa, na yasiyo ya umoja huo.

"Mwenyekiti anakubaliana na taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inayosisitiza umuhimu wa mfumo imara, athirifu, na unaojumuisha pande nyingi wakati ambapo jamii ya kimataifa inakabiliwa na changamoto za kimataifa zinazoingiliana," imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa ya AU imesema changamoto hizo zinazoikumba jamii ya mwanadamu ni pamoja na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, uchumi uliodorora, na changamoto za afya ya umma.

Mwenyekiti wa Tume ya AU amesisitiza kwamba, taasisi hizo ambazo Marekani ilijiondoa kwazo "zina jukumu muhimu katika kupiga jeki maendeleo ya Afrika, kuimarisha amani, kutatua changamoto za kibinadamu, na kufanikisha utekelezaji wa Ajenda ya 2063 ya AU na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu."

Haya yanajiri siku chache baada ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric kusema madai ya Marekani kwamba taasisi hizo za kimataifa yakiwemo mashirika 31 ya UN hazina maana tena na zinaendeshwa ndivyo sivyo haya msingi wowote.

Alisema kujiondoa Marekani kwenye taasisi hizo muhimu za kimataifa kutadhoofisha ushirikiano wa kimataifa na kupunguza uwezo wa taasisi hizo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.